Timu ya wanachuo watafiti kutoka nchini Korea inayojulikana kwa jina la AQUA.Wa kwanza kulia ni kiongozi wa jopo hilo la wanachuo (AQUA), Peter Kang akizungumzia utafiti wao juu ya huduma ya maji safi na salama.
Timu ya wanachuo watafiti kutoka nchini Korea inayojulikana kwa jina la AQUA katika picha ya pamoja na Profesa Hong Seong (wa pili kushoto) mshauri na mfadhili wa kimu hiyo kwa ushirikiano na MIT. Mratibu wa Mafunzo na Maendeleo, Denis Mnyanye kutoka 'Son International' (kushoto) akizungumza na kiongozi wa jopo hilo la wanachuo (AQUA), Peter Kang. Kiongozi wa jopo la wanachuo (AQUA), Peter Kang (wa tatu kulia) akiwatembeza baadhi ya wanahabari kuona kaya zilizopewa machujio ya kutibu maji eneo la Kiwalani, jijini Dar es Salaam.
Peter Kang (kulia) akiwa na mmoja wa akitembelea baadhi ya kaya zilizopewa machujio ya kutibu maji eneo la Kiwalani, jijini Dar es Salaam."]
Peter Kang (kulia) akiwaonesha wananchi maji ambayo yamefanyiwa utafiti na kujulikana yapo salama baada ya kuchujwa na machujio hayo. Baadhi ya wananchi wakielimishwa juu ya teknolojia hiyo leo.
BAADHI ya familia eneo la Kiwalani jijini Dar es Salaam zimenufaika na teknolojia ya kutibu maji kirahisi na kuwa safi na salama kwa matumizi ya nyumbani. Timu ya wanachuo watafiti kutoka nchini Korea inayojulikana kwa jina la AQUA ndiyo inayoratibu programu hiyo ya majaribio ya kuwezesha kaya kupata maji safi na salama kwa matumizi.
Programu hiyo inayotarajia kuenezwa maeneo mbalimbali nchini Tanzania imeanza kwa kuzipatia kaya 15 machujio rahisi yaliotengenezwa kuchuja maji na kuyatibu ili yawe safi na salama kwa matumizi ya binadamu moja kwa moja.
Akizungumza kiongozi wa jopo hilo la wanachuo (AQUA), Peter Kang alisema utafiti wao umefadhiliwa na Massachusetts Institute of Technology chini ya usimamizi wa Profesa Hong Seong hapo baadaye programu walioanzisha itasambazwa maeneo anuai ya Tanzania.
Alisema programu hiyo mbali ya kusaidia familia kupata maji safi na salama itawaondolea wanawake kero ya kusaka maji safi na salama kundi ambalo ndilo lenye majukumu ya kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia nyumbani.
Aidha alisema programu hiyo imeonekana kupokelewa kwa muitikio mzuri huku wanawake wakiwa mstari wa mbele kwani baadhi ya vikundi vimekuwa vikijipatia kipato kwa kuziuzia familia kadhaa maji hayo safi na salama baada ya kutibiwa.
Alisema hata hivyo programu hiyo imepokelewa kwa muitikio mzuri haswa na akinamama ambao kikawaida katika kaya nyingi hutimia muda mrefu kufuatilia maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Kwa sasa AQUA wametoa jumla ya machujio 15 yenye ujazo wa lita 60 kwa majaribio kwa baadhi ya kaya na kaya hizo zitatakiwa kuchangia kiasi cha shilingi elfu 5,000 kwa mwezi na baadaye watakabidhiwa umiliki wa machujio hayo moja kwa moja. Machujio hayo yanauwezo wa kuchuja na pia kuuwa wadudu hatari kwa afya ya binadamu kwenye maji na kuyaacha maji safi na salama kwa matumizi.
Naye Mratibu wa Mafunzo na Maendeleo, Denis Mnyanye kutoka 'Son International' ambao ni watengenezaji wa machujio hayo alisema teknolojia hiyo ni rahisi na salama hivyo kuomba jamii kuiunga mkono, hasa ukizingatia kiasi kikubwa cha maji yanayotumika baadhi ya maeneo nchini si salama kutokana na mazingira yetu.
"...kutokana na mfumo wetu wa usambazaji maji na miundombinu yake kuna uwezekano baadhi ya maeneo watu wakapokea maji ambayo si salama, au yale yanayopatikana baadhi ya visima lakini ukitumia machujio haya nyumbani unayatibu maji yako mwenyewe hivyo kuwa salama zaidi," alisema Mnyanye.
~Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment