Tangazo

August 19, 2013

MAAZIMIO YA MAFUNZO YA KAMATI ZA BUNGE ZINAZOSIMAMIA FEDHA ZA UMMA NA BAJETI (PAC, LAAC NA BC) YALIYOFANYIKA OCEANIC BAY HOTEL BAGAMOYO 17th AUGUST, 2013

Na Zitto Kabwe

    Kutokana na kutokuwepo na taarifa sahihi kuhusu deni la Taifa kuna umuhimu wa kukutanisha wadau wakuu wanaohusika hususani BOT, HAZINA, Kamati za Bunge na CAG ili kuweza kujua kwa usahihi zaidi ukubwa wa deni hilo.  Vile vile imeamuliwa kuwa Serikali ishauriwe kuunda chombo huru kitakachosimamia deni la taifa.

    Baada ya kuanzisha mfumo mpya wa bajeti ya Serikali mwaka huu kuna umuhimu wa kuandaa mkutano wa kutathimini mafanikio na changamoto za mfumo huu na kujadili mambo ya kuboresha zaidi mfumo mzuri wa bajeti ya Serikali.

    Kamati za Bunge zinazoshughulikia usimamizi wa fedha na rasilimali za taifa zishughulikie zaidi Maafisa Masuuli hatarishi (risk based) ili kuleta thamani ya fedha katika utendaji wao.  Kamati zishirikiane na CAG katika kuamua ni Afisa Masuuli yupi aitwe kukutana na Kamati.

    Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge na TAMISEMI waanzishe utaratibu wa kuratibu mikutano na mafunzo ya Wakurugenzi wa Halmashauri kwa pamoja kuliko kila Wizara kuwaita watendaji hao katika sehemu mbalimbali kwa muda tofauti na kuwafanya kutokuwepo ofisini kwa kipindi kirefu.

    Mfumo wa kutunza kumbukumbu za hesabu na nyaraka mbalimbali katika Serikali Kuu na Halmashauri uboreshwe ili zinapohitajika zipatikane kwa wakati muafaka bila kisingizio cha aina yoyote.

    Kuhusu ukaguzi wa ufanisi CAG asisubiri mpaka asikie malalamiko kutoka kwa wananchi au kwenye magazeti bali akague mara kwa mara sehemu zote zenye matatizo.

    Taarifa za mwaka za Kamati za Bunge ziwe na kipengele cha kiwango cha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati yaliyotolewa awali. Kamati ziwezeshwe kifedha ili ziweze kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yao. Kanuni za Bunge zieleze utaratibu wa ufuatiliaji wa Maazimio ya Bunge na namna utekelezaji wake utavyowasilishwa Bungeni.  Vile vile Bunge litenge siku ya kujadili Serikali ilivyoshughulikia hoja za Kamati za Bunge.  Spika ashauriwe kuhusu umuhimu wa kuunda Kamati ya Bunge ya kufuatilia ahadi za Serikali.

    Mikataba katika ngazi ya Serikali za Mitaa iandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

    Serikali inatakiwa kufanya jitihada za ziada kuzalisha wataalam wa fani ya manunuzi.  Kuna umuhimu wa PPRA kuongezewa nguvu za ziada za kiutendaji ikiwa ni pamoja na fedha na wafanyakazi.
    Bajeti ya Bunge iongezwe kupitia Mfuko wa Bunge na iwasilishwe Bungeni na Naibu Spika na sio Ofisi ya Waziri Mkuu.

    Serikali iandae mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na vitendo vya rushwa na mmomonyoko wa maadili vinavyoongezeka kwa kasi hapa nchini. Vilevile viongozi wa umma na watendaji waongoze kwa mfano kwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao.

    Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haiweki uwazi wa kutangaza umiliki wa mali za viongozi.  Hii inapelekea viongozi kutoweka wazi mali wanazomiliki na ni rahisi mtu kuzushiwa umiliki usio wa ukweli.  Ni vyema Sekretarieti wakafanya utafiti wa umiliki wa mali kwa viongozi wa Umma na kuweka taarifa hizo katika tovuti ya Sekretariati ili kuwawezesha wananchi kuweza kuona mali zinazomilikiwa na viongozi wao; na pale ambapo kiongozi hatakuwa ametoa taarifa ya umiliki huo basi taarifa hiyo itolewe kwa Tume.

    Kwa kuwa leseni za udereva za sasa zinaweza kuweka kumbukumbu za makosa ya usalama barabarani, basi TRA ikishirikiana na  Wizara ya Mambo ya Ndani zihakikishe ya kuwa Askari wa Usalama Barabarani wanatumia utaratibu huu wa kisasa wa kutoa  “notification” na kutoa risiti za malipo za elektroniki.

    Maduhuli ya Serikali sasa yakusanywe kwa kutumia risiti za elektroniki.  Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma yaanze kutumia risiti za eletroniki mara moja ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali yanayotokea hivi sasa katika kutumia risiti zinazoandikwa kwa mkono. Pia ofisi za serikali zifanye manunuzi yake kwa wafanyabiashara wanaotumia mashine za kielektroniki.

    TRA ihamasishe wananchi na wafanya biashara umuhimu wa matumizi ya risiti za elektroniki, wafanyabiashara waelimishwe umuhimu wa kutoa risiti hizo na wananchi waelimishwe umuhimu wa kudai risiti kila wanapofanya manunuzi. Elimu na uhamasishaji huo unaweza kufanywa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo sanaa, timu za michezo, bendi za muziki, redio, TV, mbao za matangazo n.k.

    Serikali idhibiti makampuni ya uwakala wa kupakia na kupakua mizigo (clearing and forwarding) yaliyopo Bandarini ili kudhibiti mapato ya forodha.

    Sheria ya “Anti Money Laundering” ya 2006 irekebishwe ili iweke viwango vya fedha ambazo mtu anaweza kuingia au kutoka nazo nchini bila kuzitaja  (declare). Kuna umuhimu wa Waziri wa Fedha kutengeneza kanuni za kutekeleza Sheria hiyo.

    Benki Kuu iandae mfumo thabiti wa usimamizi wa Maduka ya Fedha (Foreign Bureau de Change), na kuhakikisha kutungwa kwa sheria inayozuia matumizi ya fedha za kigeni katika shughuli za kibiashara hapa nchini.

    “The Proceeds of Crime Act, 1991” ifanyiwe marekebisho na kuweka kifungu kinachomwezesha AG/DPP kuwa na mamlaka ya kuomba mahakama kufungua kesi ya madai (Civil Forfeiture) kwa watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

    Imesisitizwa kwamba CAG akague misamaha ya kodi na kuweka taarifa hiyo kwenye taarifa za kila mwaka.

    Serikali iimarishe Taasisi zinazoshughulikia maadili utawala bora na uwajibikaji kama vile Sekretariati ya Maadili ya Viongozi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Takukuru, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Kamati ya Maadili ya Bunge ili ziweze kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizoanzisha Taasisi hizo.

    PCCB na vyombo vingine vinavyohusiana na kushughulikia masuala ya jinai wawe waalikwa kwenye vikao vya Kamati za Bunge ili waweze kutoa ushauri kwenye kamati hizo.

No comments: