Tangazo

August 6, 2013

SIYO KILA MABADILIKO YANA FAIDA:NAPE


NAPE NNAUYE
Mwanza, Tanzania 
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi, CCM, Nape Nnauye amesema japokuwa mabadiliko ni muhimu kwa maisha ya binadamu lakini lazima kila yanapohitajika yafanywe kwa umakini mkubwa ili yasiwe na madhara.

Amesema ni kutokana na sababu hiyo, ndiyo maana CCM imekuwa ikisisitiza umakini na busara kubwa vitumike wakati huu ambao Tanzania ipo katika mchakato wa kupata katiba mpya.

Nape amesema miongoni mwa mambo ambayo CCM inaona kwamba lazima yatazamwe kwa umakini na busara kubwa kabla ya hatua ya mwisho, ni kuhusu Tanzania kuwa na serikali ngapi, ambapo rasimu ya kwanza ya Katiba inapendekeza serikali tatu.

Nape ambaye alikuwa akizungumza wakati akifungua Kongamano la Vijana mkoani Mwanza lililofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu (BOT) Kapripoint jijini Mwanza, juzi, alisema, kwa upande wake CCM kuhusu kipengele hicho cha Tanzania kuwa na serikali ngapi, msimamo wake ni serikali mbili.

"Sisi CCM tunapotangaza msimamo wetu kwamba nchi hii inastahili kuwa ya serikali mbili, haina maana kwamba tunadharau au kuwaona wapuuzi  wanaopendekeza ziwe tatu, la, msimamo wetu huu tunaueleza kwa hoja ili hatimaye jamii ya Watanzania ikiziona zina mantiki watuunge mkono", alisema Nape.

Aidha Nape alisema, umuhimu wa kuwa makini na kutumia busara katika jamii kuhitaji mabadiliko unatokana na kwamba jamii ikiyapokea kwa pupa huambulia yasichotarajia, ikiwemo machafuko au uongozi wasiohitaji kwa ajili ya kukidhi matakwa yao ya maendeleo.

Nape alisema  katika pupa ya kutafuta mabadiliko, zipo baadhi ya nchi kama Misri ambazo hadi sasa zimekosa utulivu kutokana na kupokea vibaya dhana ya mabadiliko, wakaingia mitaani lakini bila kuchukua tahadhari, hatimaye wamejikuta mabadiliko waliyopata nayo hawayataki tena, wanataka mengine.

Akifafanua alisema, CCM inatambua kwamba, muundo wa serikali mbili ndio utafaa katika kudumisha Muungano, kuliko serikali tatu ambazo CCM inaona kwamba mbali ya kuwa mzigo zaidi kwa wananchi, pia ni kuongeza changamoto juu za zile zilizopo sasa kwenye muungano.

No comments: