Tangazo

September 11, 2013

NAPE:CHADEMA WAMEPEWA MABILIONI TOKA NJE KUVURUGA MCHAKATO WA KATIBA

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa Nape Nnauye akihutubia wakazi wa Kahama kwenye viwanja vya CDT na kuwaeleza mbinu chafu zinazofanyika kuvuruga mchakato wa Katiba.
  •  Adai ndio chanzo cha kupigana bungeni
  •  Asema ndizo walizotumia kuzunguka na helkopta nchini.
  •  Aeleza yaliyotokea bungeni sio bahati mbaya, Chadema waliyapanga
  •  Ashukuru bunge kuendelea kuonyeshwa"live" ili wananchi waone ujinga wao.
  •  Awatuhumu kuweka masilahi yao mbele badala ya nchi.
  •  Asisitiza CCM kuendelea kuheshimu uamuzi wa wananchi juu ya katiba.
  •  Aonyesha madai ya Chadema kitakwimu yasivyojali wakulima na wafanyakazi.

Katibu wa NEC ya CCM itikadi na Uenezi amesema kinachowasumbua Chadema mpaka wanafanya yote waliyoyafanya hasa ngumi na vurugu bungeni ni namna watakavyoeleza kwa waliowapa pesa za kuvuruga mchakato wa katiba nchini kwani wanatakiwa kupeleka mrejesho jinsi walivyofanikiwa na jinsi walivyotumia mabilioni hayo.

Nape ameyasema hayo kwenye mkutano mkubwa wa hadhara mjini Kahama kwenye ziara ya karibu siku ishirini kanda ya ziwa kwa mikoa mitatu yaani Shinyanga,Simiyu na Mara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndg. Abralhaman Kinana.

"Wenzetu hawa nasikia wamepewa mabilioni toka nje kwa kisingizio cha kushiriki mchakato wa katiba, na kama ilivyo kwa vibaraka wengine katika bara la Afrika lengo la mapesa hayo sio kuwawezesha kushiriki bali kuanzisha fujo na vurugu ili mchakato usimalizike salama iwe ajenda 2015 kwani kimsingi hawana ajenda mpya" alisisitiza Nape.

Akielezea swala la pesa kutoka nje Nape alisema mara tu baada ya rasimu ya kwanza kutoka Katibu Mkuu wa Chadema alikwenda nje ya nchi na akakaa kwa muda na aliporudi tu, ndio Chadema wakapanga kuanza kuzunguka na helkopta.

"Babu atwambie alifuata nini nje? Na pesa za kuzunguka na misafara miwili tofauti ya helkopta walitoa wapi? Na watwambie kama walisharudisha mrejesho kwa wafadhili wao" alisema Nape

Nape aliendelea kusisitiza kuwa yote yaliyotokea bungeni si mambo yaliyotokea kwa bahati mbaya isipokuwa ni mambo yaliyopangwa na Chadema katika mkakati wa kutimiza moja ya malengo yao.Alisema ilikua ni lazima watafute mahali pa kufanya kituko bungeni ili iwe mjadala na ili wapate sababu na picha za kuonyesha kwa waliowapa pesa kuwa wanapambana.

"hili walilofanya Chadema bungeni ni jambo walilopanga katika mkakati wao wa 'civil disobidiency' ...machafuko ya umma dhidi ya dola, mkakati ambao unaratibiwa kutoka nje na baadhi ya wale waliokuwa wakoloni katika nchi zetu za Afrika. Lengo ni kusababisha machafuko na nchi kutotawalika" alisema Nape.

Nape alisema ndio maana CCM ilisisitiza lazima bunge liendelee kuonyeshwa na televisheni ili kuonyesha yanayoendelea bungeni kuwawezesha wananchi kuona kinachofanywa na wawakilishi wao.
"bila shaka wananchi mmeona kilichotokea bungeni kwa macho yenu, sina haja ya kuwaeleza. Mmeona wabunge wa upinzani walichofanya,uchaguzi ujao tupunguze idadi ya vichaa bungeni ili kodi zetu zitumike vizuri,kwani tuliwatuma wakajadili maendeleo yetu wao wamegeuza bunge uwanja wa masumbwi.

Aidha Nape akifafanua hoja ya upinzani bungeni juu ya idadi ya wabunge wa bunge maalum la katiba alisema upinzani hawana hoja ya msingi bali wanasukumwa na ubinafsi na ulafi wa madaraka.
"Hoja iliyowafanya wapigane bungeni haina mashiko, wanataka idadi iongezwe ya wabunge wa bunge la katiba kutoka 357 mpaka 792. Hivi nani anabeba mzigo huu wa kuwalipa hawa wabunge kama sio mwananchi wa kawaida? Halafu mnajiita watetezi wa wanyonge? Hamuoni aibu?" alihoji Nape.

Akiendelea kufafanua Nape anasema, " katika hali ya kawaida tungetegemea wajenge hoja ya kundi kubwa katika jamii ya kitanzania ambao ni wakulima na wafanyakazi ndio wawe na uwakilishi mkubwa kwenye hilo bunge kama tunataka katiba kweli ya wananchi lakini badala yake wao wanapendekeza wawakilishi kutoka vyama vya siasa ukiacha wabunge waliopo sasa wawe 72 na wakulima wawe 10 tu! Wanataka katiba ya vyama vya siasa badala ya katiba ya nchi kwa ajili ya wananchi. Wanataka wafugaji wawe 10 tu na wafanyakazi 40. Kwa uwiano wa kawaida asilimia 80% wa wananchi wa nchi hii ni wakulima, tungetegemea wangependekeza idadi yao kuwa kubwa lakini wao wanawapuuza wakulima na wafugaji kwa kudai wawe kumi tu"!

Nape alimalizia kwa kudai kuwa siku za vyama kama Chadema zinahesabika maana hii ya katiba ndio ilikuwa karata yao ya mwisho.
" Nimalizie kwa kuwatahadharisha vijivyama hivi vingine kama CUF, NCCR mageuzi na wengine kuwa wenzao wamepewa mapesa wao wanwaunga mkono kwa ajenda iliyojificha. Na kwakuwa hili la kuvuruga katiba ndio karata yao ya mwisho basi tutarajie anguko baya sana kwa Chadema na huo ndio utakuwa mwisho wao"!alimalizia Nape.


No comments: