Na Mwandishi Wetu, Handeni
SERIKALI kwa kupitia Mkurugenzi Mtendaji wilayani Handeni,
mkoani Tanga, Dr Khalfany Haule (PICHANI), imebariki kufanyika kwa tamasha la utamaduni
la Handeni Kwetu 2013, linalotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu wilayani
humo.
Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza wilayani humo
likiwa na lengo la kukuza na kutangaza utamaduni na utalii wa Tanzania, ukiwa
ni mpango wenye mashiko kwa sekta hiyo.
Akizungumza juzi mjini hapa, Dr Haule alisema ni kitendo
kinachopaswa kuungwa mkono na serikali yote ili kuongeza kasi ya kuleta
maendeleo kwa kupitia njia mbalimbali.
Alisema wao kama wilaya wamepokea kwa mikono miwili wazo
zuri la kuandaliwa kwa tamasha hilo wilayani Handeni mkoani Tanga, hivyo
watakuwa pamoja na waandaaji.
“Tunashukuru kwa dhati kuona mwaka huu mwishoni kunafanyika
tamasha hili lenye mguso wa aina yake, maana watu watakutana kuangalia mambo ya
utamaduni wa Handeni na Tanzania kwa ujumla.
“Tupo tayari kushirikiana kwa karibu na waandaaji wa tamasha
hili ili lifanyike kwa mafanikio na kuleta ari mpya katika sekta ya maendeleo
ya Taifa, hususan wilayani Handeni,” alisema Haule.
Tamasha la Utamaduni wa Handeni linafanyika kwa mara ya
kwanza kwa kuandaliwa na Raha Company And Entertainment likiwa na malengo ya
kukuza na kutangaza sekta ya utamaduni na utalii hapa nchini na kusubiriwa kwa
hamu wilayani humo.
No comments:
Post a Comment