Tangazo

October 31, 2013

Redd’s Uni-Fashion Bash kumekucha Moshi

Na Mwandishi Wetu, Moshi

KUMEKUCHA ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro, pale wanamitindo na wabunifu walio katika vyuo vikuu watakapochuana kesho katika tamasha la ‘Redd’s Uni-Fashion Bash’, ndani ya Ukumbi wa Glessius uliopo mjini hapa.

Tamasha hilo linalochochea vipaji ndani ya vyuo hivyo, awali lilifungua pazia ndani ya Mkoa wa Mwanza na litahusisha pia vyuo vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam na Iringa.

Akizungumzia tamasha hilo, Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butallah alisema, vyuo vinne vilivyopo mkoani humo ndivyo vinavyotarajiwa kushiriki.

Wanafunzi wabunifu na wanamitindo wanaotarajiwa kushiriki tamasha hilo wanatoka Chuo Kikuu cha Mwenge, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi ya Afya Kilimanjaro, Tumaini na Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara.

Fimbo alisema, wanafunzi wa vyuo vyote vya elimu ya juu walio na mapenzi katika ubunifu na mitindo wanatarajiwa kushiriki shindano hilo, huku akiamini kutakuwa na upinzani mkali zaidi ya ule wa Mwanza. Burudani inatarajiwa kutolewa na msanii Jon Makini ‘Mwamba wa Kaskazini’.

Tamasha la awali lililofanyika Mwanza, kulikuwa na ushindani mkali katika mitindo ambapo Fahad Rajab kutoka Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT) aliibuka mshindi akifuatiwa na Lucy Charles kutoka pia chuo hicho.

Fahad kwa ushindi huo alijinyakulia Sh 500,000 huku Lucy akitwaa Sh 400,000 na mshindi wa tatu Ally Thabit wa Chuo cha Biashara (CBE) akiondoka na Sh 300,000 huku Joseph Mmari wa SAUT aliyeshika nafasi ya nne pamoja na Victoria Newton pia kutoka chuo hicho aliyeshika nafasi ya tani kila mmoja akipata Sh 100,000.

Kwa upande wa wabunifu mshindi wa kwanza alikuwa Dotto Elius wa CBE aliyejitwalia Sh 700,000, akifuatiwa na Fahad Rajab wa SAUT aliyepata Sh 500,000 akifuatiwa na Rafaka Mtani wa Taasisi ya Uhasibu (TIA) aliyeondoka na Sh 300,000.

Washindi wa nne na watano walikuwa ni Amedias Amedia wa SAUT na Elizabeth Mtani wa TIA ambao kila mmoja aliondoka na Sh 100,000.

Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema katika tamasha la leo, fedha za zawadi zitakazotolewa zitakuwa kama zile zilitolewa kwa washindi wa Mwanza.

“Tunataka kuinua vipaji vya wanafunzi wa vyuo katika tasnia ya mitindo, kwa sasa wanafunzi katika mikoa iliyobaki wanatakiwa wajiandae mno, maana kuna upinzani mkubwa,” alisema Edith.

Kinywaji cha Redd’s Original pia ndicho kinachodhamini shindano la Redd’s Miss Tanzania na kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
 

No comments: