Tangazo

November 6, 2013

TAASISI YA WAMA INATARAJIA KUFANYA KAZI KWA PAMOJA NA UTEPE WA PINKI UTEPE MWEKUNDU KUKABILIANA NA UGONJWA WA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI NA MATITI

Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda- Maelezo

 Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na Utepe wa Pink Utepe Mwekundu (PRRR) wanatarajia kuanza kufanya kazi kwa pamoja ya kuhakikisha kuwa ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi na matiti unapungua  au kuisha kabisa hapa nchini .

Hayo yamebainishwa  wakati wa mazungumzo baina ya Wafanyakazi wa Taasisi ya WAMA wakiongozwa na Mwenyekiti wao  Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na Ujumbe kutoka Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu yaliyofanyika katika ofisi za  WAMA zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji kutoka Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu Dk. Doyin Oluwole alisema  jambo la muhimu ni kuangalia jinsi gani wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kuudhibiti ugonjwa huo ambao unawatesa wanawake wengi hapa nchini.

“Ili kukabiliana na  ugonjwa huu  Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa dharula wa kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU)  na Ukimwi (PEPFAR) imetoa  dola za kimarekani millioni tatu kwa kipindi cha miaka mitano na mashine 16 za cryotherapy kwa ajili ya kusambaza huduma za upimaji na tiba kwa wanawake wenye ugonjwa saratani ya shingo ya kizazi”, alisema Dk, Doyin.

Pia kwa kipindi cha miaka mitatu  Shirika la Misaada la Marekani (UNAIDS) limetoa dola 33,000 kwa ajili ya kusaidia ushiriki wa wanawake wenye VVU na kufanya kazi na vikundi vidogovidogo katika jamii. Taasisi ya Bristol –Myers Squibb kwa kipindi cha miaka  mitatu imetoa dola za kimarekani milioni 1.2 kwa ajili ya kusaidia huduma za kuhamasisha jamii kuhusu  vikoba na kuimarisha huduma za jamii.

Alisema watashirikiana kwa kila hali ili kuhakikisha kuwa wanawake wa Tanzania wanapata matibabu ya ugonjwa huo lakini hawawezi kufanya kazi peke yao  bila ya  Mama Kikwete kwani  yeye ni mama wa taifa, akiongea na  wanawake watamsikiliza.

Aidha Dk. Oluwole pia alimpongea mama Kikwete pamoja na mmewe Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwasaidia watanzania.

Dk. Doyin alisema, “Tunakupongeza kwa kazi kubwa unayoifanya ya kutumia sauti yako kuwaelimisha watanzania kuhusiana na mambo mbalimbali ya maendeleo, kuhusu ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti sisi tukiongea na watanzania hawatatuelewa kama vile wewe ukisimama na kuongea nao”.

Kwa upande wake Mama Kikwete aliishukuru Serikali ya Marekani kwa misaada mingi wanayoitoa kwa wananchi wa Tanzania na kusema kama ushirikiano huo utaanza kufanya kazi mapema itakuwa ni rahisi kuweka kukabiliana na ugonjwa huo ambao unaua wanawake wengi hapa nchini.

Mama Kikwete alisema hivi sasa maambuki ya Ugonjwa wa Ukimwi yamepungua kwa asilimia 5.1 lakini kuna mikoa ambayo bado maambukizi yako juu kama mkoa wa Njombe kwa asilimia 14.8, Iringa, Mbeya na Mwanza.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema changamoto iliyopo ni kuwa mtu mwenye viashiria vya kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ana hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU  hali hiyo haiwezi kufumbiwa macho ni lazima  ipatiwe ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano jambo ambalo  litapunguza  tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.

“Tunatambua kwamba saratani ya shingo ya kizazi inaua wanawake wengi hapa nchini , mwanamke anakitu kinaitwa usiri anaweza kupata tatizo akakaa nalo kwa muda mrefu na kuona aibu kulisema ingawa inaweza kutokea kwa bahati mbaya mtu mwingine akaona kuwa kuna tatizo  lakini bado mwanamke huyo akashindwa kusema.

Ni muhimu tukawaelimisha wanawake wakajua kuna ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti , tatizo si kujua tatizo lililopo  bali tatizo ni kuficha ugonjwa naamini  wakati umefika wa kulifanyia kazi jambo hili ni muhimu  kuangalia mahali  ambako kuna tatizo kubwa zaidi  na kupeleka  utetezi kwa wahusika kwani maisha bora ya watanzania yanategemea kuimarika kwa afya zao nchi ikiwa na watu wenye afya njema kutakuwa na kizazi chema pamoja na viongozi wazuri hapo baadaye”, alisema Mama Kikwete.

Utepe wa Pink Utepe Mweupe  ni muungano wa  mashirika ya kiserikali na  yale yasiyo ya Kiserikali ya nchini Marekani wenye malengo yanayofanana ya kupunguza vifo vitokanavyo na saratani ya shingo ya uzazi na ile ya matiti katika nchi zenye uchumi wa chini na ule wa kati. Washirika wa muungano huo ni Chuo cha George W. Bush, PEPFAR, UNAIDS, Susan G Komen, Becton Dickinson na Kampuni yake, Taasisi za a Bill ma Melinda Gates, Bristol Meyers Squibb na Caris, IBM, Merck , Qiagen, Taasisi ya Taifa ya Saratani, Medisend, AirBarneLife Line, MD Anderson, Jamii ya Kansa ya Marekani na American Society for Clinical Pathology.

Tanzania ni nchi ya tatu katika nchi za Afrika kuingia kwenye urafiki na Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu ambao ulizinduliwa na Rais Dk. Kikwete na Rais Mstaafu wa Marekani George W. Bush kwenye  mkutano wa wake wa Marais wa Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwaka huu. Utafanya  kazi chini ya uongozi  wa  mkakati wa taifa wa upimaji na uzuiaji wa saratani ya shingo ya uzazi na dira ya wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

No comments: