Tangazo

December 7, 2013

Security Group yakumbwa na kashfa


 KAMPUNI ya ulinzi ya kimataifa ya Security Group, ambayo inatoa huduma ya ulinzi kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa (U.N), mabalozi, mabenki na ofisi nyingine kubwa nchini, inadaiwa kukwepa kodi na kujiendesha kiujanjaujanja, Tanzania Daima limebaini.

Kampuni hiyo maarufu nchini, inadaiwa kujiendesha kiujanja kwa kuajiri wafanyakazi wachache na wengine kuwakodi kwa ujira mdogo kutoka makampuni mengine binafsi ya ulinzi ya hapa nchini.

Uchunguzi umebaini kuwa wafanyakazi wanaokodishwa, huvalishwa sare za Security Group ili kukwepa kodi na gharama za uendeshaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema Security Group Tanzania yenye wafanyakazi takriban 300, imekuwa ikitumia zaidi ya wafanyakazi 1,000 kutoka kampuni za ulinzi za Kitanzania kwa kuwavalisha sare zake na kuwaweka walinde ofisi zilizoingia mkataba nazo bila kujali kama wana sifa au la.

Aidha walisema kuwa uongozi wa Security Group umeondoa wafanyakazi wote wanaotakiwa kushika silaha ili kukwepa kuwalipa mshahara wa sh 300,000 kwa mwezi kwa mujibu wa sheria ambapo wameamua kukodi wafanyakazi wasio na sifa kutoka kampuni binafsi ili waweze kuwalipa mshahara mdogo wa sh 180,000 kwa mwezi.

Mmoja wa wafanyakazi wa kukodi toka kampuni binafsi ya ulinzi ya GPS Security Limited, yenye maskani yake katika eneo la Kawe Kanisani jijini Dar es Salaam, Ally Maulid, ambaye kwa sasa anaitumikia kampuni ya Security Group katika kitengo cha kulinda silaha, alisema anashangazwa kuona wanapewa dhamana kubwa ya kufanya kazi ya ulinzi katika malindo muhimu kama mabenki na mabalozi bila kuwa na mikataba yoyote ya ajira.

Aidha Maulid anabainisha kuwa kilichofanyika ni wao kukabidhiwa sare za Security Group na silaha aina ya bunduki kisha kuaminiwa na kupelekwa kulinda katika malindo nyeti na muhimu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao na kwa wateja wanaolindwa.

Kwa mfano hapa unaponiona nimevaa sare za Security Group, lakini mfukoni kwangu nina kitambulisho cha GPS Security Limited, sina ajira na GPS zaidi ya hiki kitambulisho tu walichonipa sasa nikitaka kufanya uhalifu hapa watanipata wapi?” alihoji Maulid.

Aidha uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kampuni hiyo imekuwa ikiweka walinzi wawili, mmoja mwajiriwa wa Security Group ambaye haruhusiwi kubeba silaha na mwingine wa kukodi ambaye ndiye mwenye dhamana ya kubeba silaha.

“Mimi hapa nimepewa dhamana ya kulinda na silaha licha ya kuwa sina ajira lakini mshahara wangu ni mdogo, nalipwa sh 180,000 kwa mwezi wakati mwenzangu niliyenaye lindo moja na ameajiriwa analipwa sh 240,000 sasa, uliona wapi kama si kutuweka majaribuni?” alihoji Maulid.

“Kwa hiyo kampuni ya Security Group inalipwa mabilioni ya shilingi kwa kuwachaji wateja wake kama kampuni ya kimataifa wakati inatumia walinzi wa kampuni za Kitanzania ambao wengi hawana sifa ili kukwepa kuwalipa mishahara stahiki,” alisema Maulid.

Aidha makampuni mengine ya ulinzi ya Kitanzania yanayoshirikiana na Security group ukiacha kampuni ya Iron Side yenye wafanyakazi zaidi ya 700 wanaovalishwa sare nyingine ni pamoja na Insight Security na GPS Security Ltd.

Kwa mujibu wa sheria za nchi, makampuni ya ulinzi ya kimataifa yanatakiwa yawalipe wafanyakazi wao mshahara wa juu kuliko makampuni ya ulinzi ya Kitanzania.

Akijibu tuhuma hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Dominique Ooko, alisema kampuni yake ni moja ya makampuni yanayolipa kodi bila ya matatizo.

“Kama unataka kujua ukweli kuhusu kampuni yetu inalipia wafanyakazi wangapi walioajiriwa nakuomha uende NSSF uwaulize, kwa kuwa mimi nikisema utadhani nasema uongo.

“Aliwahi kuja mwenzenu kuuliza swali kama hili tukamuomba atuletee kwa maandishi na tukamjibu sasa kwa kuwa wewe ni mwaandishi na unataka kujua ukweli hebu fanya uchunguzi uweze kupata uhakika lakini hata ukienda TRA ukiwauliza kuhusu kampuni yetu watakwambia sisi ni walipaji kodi wazuri tu,” alisema Dominique.

Alisema kampuni yao haiwezi kukwepa kulipa kodi kwa kuwa inajua maana ya kodi na madai kwamba inakodi wafanyakazi toka kampuni zingine, sio sahihi.
Chanzo Tanzania Daima 06/12/2013

No comments: