Tangazo

February 13, 2014

FIFA YAMRUHUSU OKWI KUCHEZA YANGA

Ruksa; Okwi katikati akiwa na wachezaji wenzake wa Yanga, Juma Kaseja kulia na Hamisi Kiiza kushoto. FIFA imemruhusu kuchezea Yanga.
 
XXXXXXXXXXXXX
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limemuidhinisha mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi kuchezea klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.

Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa ameiambia BIN ZUBEIRY muda huu kwamba, FIFA imewaandikia barua ikiwaambia Okwi ni halali kuchezea Yanga SC.

“Suala la Okwi limekwisha, ila siwezi kuzungumza zaidi kwa sasa naingia kwenye kikao, tutatuma taarifa kwa vyombo vya habari baadaye,”alisema Mwesigwa.

Januari 22 mwaka huu ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilisimamisha usajili wa Mganda huyo Yanga ili kwanza upatikane ufafanuzi kutoka FIFA juu ya uhalali wake kucheza timu hiyo ya Jangwani akiwa anatambulika kama mchezaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Januari 22, mwaka huu kupitia masuala mbalimbali, ilisema imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.

Okwi ambaye aliingia kwenye mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.

Kulikuwa kuna kesi tatu FIFA kuhusiana na suala la mchezaji huyo, Okwi ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.

Hivyo, TFF iliiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake na majibu yamewasili TFF Mganda huyo akihalalishwa kuendelea na kazi Yanga.

No comments: