Tangazo

July 25, 2014

Twanga kuwatambulisha waliotoka Extra Bongo na Malaika Band Idd Mosi ndani ya Mango Garden

Luiza Mbutu
Na Daily Mitikasi Blog

BENDI ya African Stars’ Wana Twanga Pepeta, itawatambulisha rasmi wanenguaji wake wanne waliotoka bendi ya Extra Bongo na bendi ya Malaika siku ya Idd Mosi kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni.
Hayo yalisemwa na Kiongozi wa Bendi hiyo Luizer Mbutu kwenye mazoezi ya bendi hiyo yanaoyendelea kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni jana.

Mbutu aliwataja wanenguaji hao kuwa ni Maria Soloma, Sabrina Mathew, Hamza Mapande aka Dogo White na Isaack Burhani maarufu kwa jina la Danger Boy. Mnenguaji aliyetokea bendi ya Malaika ni Juma Makokoro.

Mbutu alisema kuwa sambamba na wanenguaji hao, bendi hiyo pia itawatambulisha rasmi wanenguaji wake waliorejea tena katika Bendi hiyo baada ya kurudi nchini toka falme za kiarabu walikokwenda katika ziara ya kimuziki. Wanenguaji hao ni Betty Mwangosi “Baby Tall” na Fetty Kibororoni. Na Aisha Lokolee akirejea stejini baada ya likizo ya muda mrefu.

Alisema kuwa wanenguaji hao wataungana na wale wa zamani akina Sabrina Pazi, Hamida Ibrahim, Stella “Kigoli’ Manyanya, Esta “Black American” Fred kwa upande wa wanawake ambapo kwa upande wanaume ni Mandela, Abdillahi Mzungu, Saidi ‘Dogo S” na Isihaka Idd maarufu kama Maganize.

Alisema kuwa bendi yao imejidhatiti vilivyo baada ya kupata Mau Kasibili ambaye anapiga gitaa la bass akiziba nafasi iliyoachwa na Jojoo Jumanne.

“Tumejiandaa vizuri wakati wa shoo za Idd, tuna nyimbo mpya ambazo tunazifanyia kazi na rap nyingi kutoka kwa Jumanne ‘J4’ Saidi na Dogo Rama, sisi ndiyo kisima cha burudani,” alisema Mbutu.

Akizungumzia kurejea kwao, Maria Soloma alisema kuwa wamerudi nyumbani baada ya ‘kupotea njia’ na wanajutia maamuzi yao ya awali.

“Tunatafuta maslahi, lakini kule tulipokwenda, mambo yalikuwa tofauti, tunashukuru kupokelewa tena na mkurugenzi wetu, Asha Baraka,” alisema Maria.

No comments: