xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema
kuwa moja ya sababu kubwa zinazokwamisha maendeleo makubwa zaidi na ya haraka zaidi
ya Afrika ni uzalishaji mdogo na matumizi ya chini mno ya umeme.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa hali hiyo inaeleza jinsi ongezeko la uzalishaji na
matumizi ya umeme linavyoweza kuharakisha maendeleo ya Afrika na kuleta manufaa
ya dhahiri kwa kila familia na kwa kila Mwafrika.
Rais
Kikwete ameyasema hayo jana, Jumatano, Agosti 6, 2014, wakati alipozungumza
kwenye Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi za Bara la Afrika uliofanyika chini
ya uenyekiti wa Rais Barack Obama, ambaye ni mwenyeji wa Mkutano huo.
Rais
Kikwete amewaambia wakuu wa nchi hizo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya
Mambo ya Nje ya Marekani kuwa ni dhahiri kuwa bila ongezeko kubwa la uzalishaji
na matumizi ya umeme Bara la Afrika halitatoka kwenye uduni.
Rais
amesema kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Kanda ya Shirika la Umoja wa Mataifa
Mazingira (UNEP) “Efficient Lighting in Sub Saharan African Countries” matumizi
ya umeme katika Bara zima la Afrika ni asilimia 31 tu na hivyo kulifanya Bara
la Afrika kutumia asilimia tatu tu ya umeme wote duniani.
Rais
Kikwete amesema kuwa ili kuelewa udogo wa matumizi ya umeme ya Bara la Afrika
ni kuangalia matumizi ya nishani hiyo kwa kila mkazi wa Bara hilo na yule wa
Marekani. Amesema kuwa wakati kila raia
wa Marekani anatumia kilowati 13, 246 katika Afrika wastani ni kilowati 440.
Ameongeza
Rais Kikwete: “Ukiondoa Afrika Kusini, matumizi ya umeme kwa kila raia wa Afrika
yanateremka na kufikia kilowati 160 tu.”
Amefafanua
Rais Kikwete: “Uzalishaji wa jumla wa umeme wa Bara la Afrika ni gigawati 63 ambazo
ni sawa na umeme unaozalishwa na nchi moja tu ya Ulaya – Hispania. Ukiondoa
Afrika Kusini, nchi zinazobakia wa Afrika zina uwezo wa kuzalisha gigawati 28
tu, kiasi ambacho kinazalishwa na nchi moja tu ya Marekani Kusini ya
Argentina.”
Rais
Kikwete ambaye alikuwa anafafanua jinsi utoaji huduma ulio dhahiri unavyoweza
kunufaisha wananchi na kujenga mazingira ya taasisi zisizokuwa za kiserikali
kushamiri, ametaja mambo mengine ya msingi ambayo ni lazima yawepo ili wananchi
waweze kunufaika ikiwemo elimu, ushamiri wa sekta binafsi, sera sahihi za
kiuchumi, uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa kilimo.
Pia
Rais Kikwete ametaja mambo mengine muhimu yanayoweza kusaidia kuboresha maisha
ya wananchi kuwa ni uendelezaji na matumizi ya teknolojia ya habari na
mawasiliano pamoja na kulea na kukuza demokrasia, utawala bora na utawala wa
sheria.
Rais
Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani,
anaondoka mjini Washington, D.C., leo kwenda Houston ambako atafungua na
kushiriki katika mkutano wa uwekezaji katika uchumi wa Tanzania.
Imetolewa na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
07
Agosti, 2014
No comments:
Post a Comment