NA MWANDISHI WETU,
DAR ES SALAAM
MRATIBU Mkuu wa Tamasha
la Utamaduni Handeni, maarufu kama ‘Handeni Kwetu’, Kambi Mbwana (pichani),
ameapa kuhakikisha kuwa tamasha lao msimu wa 2014 linakuwa la aina yake na
kuvunja rekodi ya mwaka jana lilipofanyika kwa mara ya kwanza wilayani Handeni,
mkoani Tanga.
Akizungumza jana jijini
Dar es Salaam, Mbwana alisema kuwa hiyo ni kutokana na kutamani kushirikisha
wasanii wengi kutoka Tanga na Tanzania kwa ujumla.
Alisema kwamba mwaka
jana wasanii zaidi ya 200 walionyesha uwezo wao kutoka kwa vikundi mbalimbali
vya wilayani Handeni na jijini Dar es Salaam.
“Mwaka jana vikundi
zaidi ya 10 vyenye wasanii wasiopungua 15 walipata nafasi ya kupanda jukwaani
kuonyesha vipaji vyao, ukiacha wasanii wanaotoka kwenye Kambi ya jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) wa Mgambo waliozidi 80.
“Wakati tunajivunia
mafanikio haya, tunaamini msimu huu utakuwa mzuri zaidi tukiamini kuwa
tutavunja rekodi ya mwaka jana, ambapo tulishuhudia burudani mbalimbali,
ikiwamo hadithi zilizohusu watu wa Handeni, bila kusahau vyakula vya asili
pamoja na michezo waliyokuwa wakicheza wazee wetu enzi hizo,” alisema Mbwana.
Kwa mujibu wa Mbwana,
mipango ya kuboresha tamasha hilo imepamba moto ambapo kwa sasa utafiti wa
ubora wa vikundi nje ya wilaya ya Handeni inafanywa ili kuhakikisha kuwa
wasanii watakaopanda jukwaani wanakuwa na uwezo wa juu na kufanikisha kwa dhati
kukuza sekta ya utamaduni pamoja na uchumi wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment