Tangazo

November 3, 2014

HOSPITALI YA KAIRUKI YAPATA TUZO YA UBORESHAJI VIWANGO VYA HUDUMA YA AFYA

 Mkurugenzi Mkuu wa Hospital ya Kairuki, Dk. Asser Mchomvu akiwa amebeba tuzo aliyokabidhiwa na na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal (katikati). Kushoto ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid.
Picha ya pamoja.

Na Mwandishi Wetu 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, ameukabidhi uongozi wa Hospitali ya Kairuki (KH) tuzo ya waliofanya vizuri katika vigezo mbalimbali vya uboreshaji viwango vya huduma ya Afya katika mkutano wa 4 wa kitaifa kuhusu uboreshaji Viwango vya huduma ya Afya uliofanyika wiki iliyopita (Octoba 31-2014) katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Hospital ya Kairuki, Dk. Asser Mchomvu alisema sifa ya mafanikio yao mpaka wakapata tuzo hiyo yanatokana na mafunzo  kwa wafanyakazi wa Hospital wapatao 20 yaliyoendeshwa na Wizara ya afya ikishirikiana na Jhpiego,CDC na PEPFAR.

Dk. Mchomvu aliongeza kuwa mafunzo kuendelea kutolewa na wakufunzi wa ndani (inhouse training), kuundwa kwa timu maalum ya ndani kwa ajili kufanya ukaguzi wa kushtukiza ndani na utayari wa KH kushirikia katika zoezi la udhibiti na uzuiaji wa maambukizi.

Aidha, Dk. Mchomvu alieleza kuwa siri nyingine ni ushirikiano mzuri baina ya manegimenti ya KH na timu ya wakaguzi toka wizara ya Afya katika kutekeleza maagizo na mapendekezo na kuyafanyia kazi.

“Kwa upande wetu maeneo yaliyofanya vizuri katika zoezi ili ni pamoja na mashine bora za kuuwa vijidudu (sterilization unit) na eneo zima katika kitengo hicho, eneo la kuifadhi/ kutenganisha na usafirishaji wa taka hatarishi, taka mbichi na taka mchanganyiko pia chumba cha upasuaji kufuata taratibu stahiki za kimataifa katika kuzithibiti maambukizi,” alisema Dk. Mchomvu.

Aliongeza kuwa wakati huohuo KH imezindua kampeni maalum za muda mrefu katika kuchunguza na kutibu magonjwa yasiyoambukiza, mfano saratani ya matiti, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya tezi dume (prostate). Saratani hizi ndizo zinazoongoza kwa  hapa nchini.
Moja ya mashine za kisasa za kupima saratani ya matiti katika Hospitali ya Kairuki.

“Lakini pia KH imezidi kuboresha huduma katika vitengo vya macho, sikio, pua na  koo kwa kupata mitambo ya kisasa katika nyanja hizo,” alisema Dk. Mchomvu.

Aliongeza kwa kusema kuwa KH imezindua wodi mpya ya kisasa hasa kwa ajili ya wanachama  wa mfuko wa Bima ya taifa ya afya. (NHIF) na wodi maalum ya watoto.

Wengine waliotunukiwa tuzo hizo za uboreshaji wa huduma za afya ni Hospitali ya Bugando-Mwanza pamoja na Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC). 

Tuzo hizo zilitolewa na Wizara ya Afya wakishirikiana na Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Marekani (CDC) na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR).

No comments: