Na Anna Nkinda – Maelezo,
aliyekuwa Nachingwea
WANAWAKE
nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kugombea
nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,
Vijiji na Vitongoji utakaofanyika
mwishoni mwa mwaka huu ili waweze kuingia
katika ngazi ya maamuzi.
Mwito huo umetolewa
jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanachama wa chama
hicho wa wilaya ya Nachingwea waliofika kumpokea mara baada ya kuwasili
wilayani humo.
Mama Kikwete ambaye ni
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema ili jambo linalowahusu wanawake liweze
kufanyiwa kazi ni lazima wawepo wanawake wenzao wa kuwapigania na hayo yote yatawezekana kama watajitokeza kuwania nafasi za uongozi.
“Ni vizuri wanawake tukakaa
kwa pamoja na kuangalia maslahi yetu kama wanawake,
katika hili hatuwezi kushinda kama siku ya uchaguzi tutakaa majumbani tu
na kutegemea watu wengine watuchagulie viongozi ni lazima siku hiyo tuende kupiga kura”, alisema Mama Kikwete.
Alisema CCM imeweza
kutekeleza Ilani yake ya mwaka 2005/15 kwa
waliyoyapanga na wasiyo yapanga hivyo
basi wanachama wa chama hicho wanakila sababu ya kutembea kifua mbele na kutoa
mfano kwa mambo yasiyokuwa katika Ilani hiyo ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambacho hadi sasa
kimeshatoa wahitimu wa fani mbalimbali.
Kuhusu mapendekezo ya Katiba
mpya MNEC huyo alisema haikuwa katika Ilani ya Chama hicho lakini kwa kuwa
Mwenyekiti wake Rais Dkt. Kikwete ni msikivu aliweza kusikia maoni ya wananchi
na kuyafanyia kazi na hapo ndipo mchakato wa kuipata katiba mpya na iliyo bora
ukaanza.
Mama Kikwete
alisisitiza, “Siku si nyingi rasimu ya katiba iliyopendekezwa itapelekwa kwa
wananchi kwa ajili ya kuipigia kura , wakati huo ukifika angalieni maslahi ya Taifa na siyo maslahi yenu binafsi
na mpige kura ya ndiyo ili tupate katiba
bora”.
Mama Kikwete alikuwa
wilayani humo kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha kamati ya siasa mkoa , wilaya
na makatibu wa CCM kata wilaya ya Nachingwea ambacho kilichojadili mambo
mbalimbali yanayohusu chama hicho.
No comments:
Post a Comment