Na Johary Kachwamba-MAELEZO
TAKWIMU zinaonesha kwamba watoto 130000
wana maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) kati ya hao 39317 wamefikiwa na
kupatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana (pichani) wakati akifungua kongamano
la nne la kitaifa la VVU na UKIMWI kwa
watoto linalofanyika katika Ukumbi wa mikutano
wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo jijini Dar-es-salaam.
Dkt . Chana alisema asilimia 39 ya
watoto walio katika hatari ya kupata maambukii ya UKIMWI hupimwa vipimo vya kubaini maambukizi
ya VVU ndani ya miezi miwili baada ya kuzaliwa hivyo basi kuna umuhimu kwa watoto hawa kupata huduma za tiba
mapema.
Akizungumzia maambukizo ya VVU kutoka
kwa mama kwenda kwa mtoto waziri huyo alisema Tanzania imepiga hatua katika
kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lengo likiwa ni kutokomeza kabisa maambukizi mapya kwa
watoto wachanga.
“Mama wajawazito na wale
wanaonyoyesha wanapatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya VVU mara tu
wanapogundulika kuwa na maambukizo, kupitia mpango mpya unaojulikana kama
‘uwezekano namba 2 au (Option B+)”, alisema Dkt.Chana.
Alisema kufikia mwezi Juni mwaka huu jumla ya akina mama 940900 kati ya 1050043 hii
ni sawa na asilimia 89.6% ya waliohudhuria kliniki walipimwa UKIMWI kati ya hao
47856 takribani asilimia 5 walikutwa na maambukizi ya VVU.
Kwa upande wa watoto 20569 walipima
kipimo cha DBS kati ya hao 2063 hii ni sawa na asilimia 10 walikutwa na maambukizo
ya VVU.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, Dkt. Donan Mbando, alisema ingawa nchi imepiga hatua katika
mapambano ya kudhibiti UKIMWI hali
halisi inaonyesha kuwa bado kuna maambukizo yanatokea sio tu
kwa watu wazima bali na kwa watoto pia.
“Ni jukumu letu kuendelea kuweka
mikakati ya dhati na kuisimamia ili kuhakikisha lengo la kutokomeza maambukizo
ya VVU tunalifikia kwani mwaka 1986 maambukizi yalikuwa juu kwa asailimia 18
lakini hivi sasa yameshuka na kufikia asilimia 5.3”, alisema Dkt. Mbando.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufundi kutoka Taasisi ya
Elizabeth Glaser Pediatric Aids (EGPAF) ambao ni waandaaji wa kongamano hilo Chrispin Kimario alisema ni muhimu kwa wazazi
na jamii kushirikiana kwa pamoja na kulibeba jukumu la kuhakikisha kila mama mjamzito anapata huduma
ya vipimo husika na matibabu kwa wakati.
Kimario alisema, “Watoto wameachwa
nyuma, ni vyema tukumbuke kuwa mtoto hawawezi kujipeleka wenyewe hospitali
kupima afya zao, hivyo ni jukumu letu wazazi, walezi na jamii kwa ujumla
kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma wanazostahili”.
Kauli mbiu ya kongamano hilo la siku
mbili ambalo limehudhuriwa na wadau wa afya kutoka asasi za umma na binafsi za
ndani na nje ya nchi ni ongeza kasi: Rahisisha upatikanaji wa utumiaji wa
huduma za VVU na Ukimwi, pata matokeo chanya ya afya za mama na watoto
wanaoishi na VVU.
No comments:
Post a Comment