Tangazo

December 25, 2014

Bingwa kati ya Msondo na Sikinde kujulikana leo TCC Club


Na Mwandishi Wetu

NANI zaidi kati ya mahasimu wa muziki wa dansi nchini Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra (Sikinde) itajulikana leo wakati miamba hao wa muziki wa dansi watapambana kwenye ukumbi wa TCC Club Chang’ombe.


Mashabiki wa bendi hizo wanatarajia kumiminika kwa wingi kushuhudia mtanange huo ambayo pia itatumika kusherekea Sikukuu ya Krismasi.


Pambano hilo linatarajia kuanzia mchana, linafanyika siku chache tu baada ya mechi ya Mtani Jembe kati ya Simba na Yanga kwa mchezo wa soka, hivyo bendi hizo nazo kuamua kuweka Nani Mtane Jembe yao kwa upande wa muziki wa dansi.


Mratibu wa pambano hilo Joseph Kapinga amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na kinachosubiriwa ni mpambano huo ambao umeandaliwa na Keen Arts na Bob Entertainment na kudhaminiwa na kinywaji cha Konyagi.


Mratibu huyo amesema pambano hilo litakuwa la kusherekea sikukuu ya Krismasi na kufunga mwaka 2014.
Kapinga alisema waamuzi katika pambano hilo watakuwa ni wanamuziki wa zamani ambao hawajawahi kupigia bendi hizo ili kuzuia upendeleo wowote.


Mmoja wa wanamuziki wa Sikinde Ngoma ya Ukae Hassan Rehani Bitchuka amesema kuwa wamejiandaa kuachia makombora makali ambayo yatawasambararisha kabisa Msondo Ngoma na wasirudie tena kupambana nao.


Hata hivyo, mwanamiziki mkongwe na bendi ya Msondo Shaaban Dede amesema kuwa siku zote Sikinde ni watoto wao, kwani imetoka ubavuni mwao, hivyo hawaoni sababu ya kushindwa kuibuka wababe kwenye pambano hilo.


Kabla ya mtifuano huo bendi ya kongwe nyingine, Vijana Jazz Wana ‘Saga Rhumba’ itatumbuiza.


Bendi hiyo itakuwa chini ya binti wa aliyekuwa kiongozi wa bendi hiyo Hemed Maneti, Komweta Maneti ambaye ataimba nyimbo zote zilizokuwa zikiimbwa na baba yake.


Kapinga alisema kuwa pia pambano hilo litaamua ni bendi gani bora kati ya magwiji hao wawili wa muziki wa dansi nchini kwa mwaka huu wa 2014.


Mratibu Kapinga alisema kila bendi itapiga kwenye jukwaa lake ili kuondoa malalamiko ya kuhujumiwa.

“Tutakuwa na michezo aina mbalimbali ya watoto kwa ajili ya kusherehekea Krisimasi,” alisema Kapinga.
 

Alisema mchuano huo utaanza saa nane mchana hadi liamba.

Wadhamini wengine wa shindano hilo ni pamoja ni Fredito Entertainmernt na Saluti5.

No comments: