Na Mwandishi Wetu
TUZO za Wanamichezo Bora wa Tanzania zinazotolewa
na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zinatarajiwa
kufanyika Desemba 12 mwaka huu, huku Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group
Limited ikijitokeza kuwa mdhamini mshiriki wa tuzo hizo kwa kutoa Sh. Milioni 10.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa
wa City Sports Lounge, Dar es Salaam katika hafla ya kutangaza udhamini huo
jana, Meneja Mkuu wa SSB Limited, Said Muhammad Said alisema wameamua kudhamini
tuzo hizo kama hatua mojawapo ya kuinua michezo nchini.
Aliupongeza uongozi wa TASWA kwa juhudi kubwa
inazofanya katika kuhamasisha michezo na kwamba wameona waunge mkono juhudi
hizo kwa kutoa fedha hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto
alisema kampuni mbalimbali zimeonesha nia ya kudhamini tuzo hizo na watakuwa
wanazitangaza kadri watakavyomalizana nazo.
“Tunaishuku sana Bakhressa kwa mchango huu mkubwa
kwetu, pia tunaomba wadau tushirikiane kwa kila hali kuhakikisha tuzo zetu
zinafanikiwa na tunaomba kampuni zaidi zijitokeze.
“Bajeti ya tuzo zetu ni Sh milioni 120, zipo
kampuni zimeonesha nia ya kutusaidia, mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa
wiki ijayo tutatangaza wadhamini wengine,” alisema Pinto.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TASWA,
Amir Mhando alisema Kamati Maalum ya Tuzo hizo inaendelea na mchakato wake wa
kupata wanamichezo hao na kwamba kadri watakavyokuwa wanapiga hatua watatoa
taarifa kwa wanahabari.
Alisema maandalizi mengine yanaenda vizuri na
wanaamini zitakuwa tuzo bora kuliko zote zilizowahi kufanywa na chama hicho
katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa miaka mitano iliyopita walioshinda
Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni
Samson Ramadhani (2006), Martin
Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni wanariadha,
wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan na mwaka 2011
alikuwa beki Shomari Kapombe ambaye sherehe za kumkabidhi tuzo zilifanyika Juni
mwaka 2012. Mwaka jana tuzo hizo hazikufanyika.
Wakati huohuo, Mhando alisema chama
chake kinaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali kuhusiana na tamasha
kwa ajili ya vyombo vya habari ‘Media Day Bonanza’ na kwamba mapema mwezi ujao
suala hilo litakuwa limemalizika.
No comments:
Post a Comment