Na Anna Nkinda - Maelezo , Nachingwea
JUMLA ya
mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.9 zimetolewa kwa wanachama wa
vikundi vya kukopa na kuweka akiba vilivyopo chini ya mradi wa Mwanamke Mwezeshe
unaosimamiwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (pichani), wakati wa
sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa kuanzishwa kwa vikundi vya mradi wa Mwanamke
Mwezeshe zilizofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Ualimu Nachingwea
mkoani Lindi.
Mama Kikwete ambaye ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema fedha zilizotolewa katika mkopo huo zimevuka lengo la kutoa mikopo yenye thamani ya
shilingi milioni 534 kwa mwaka na katika wilaya ya Nachingwea mikopo yenye
thamani ya shilingi 326,442,464/= ilitolewa.
“Kutokana na kilio cha
wanawake wengi na wafanyabiashara wadogo wadogo cha ukosefu wa mikopo yenye
masharti naafuu mradi huu ulianzishwa na kuwawezesha wanavikundi vya hisa kukopeshana kwa masharti naafuu ikiwemo kiasi
kidogo cha ziada ya mkopo ambayo kwa
lugha ya kibenki huitwa riba”, alisema.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alifafanua kuwa mradi wa Mwanamke
Mwezeshe ambao ulianza kufanya shughuli
za kijamii mwanzoni mwa mwaka jana katika wilaya za Rufiji, Kilwa, Liwale,
Lindi vijijini, Nachingwea kwa ufadhili wa Financial Sector Deeping Trust
(FSDT) unalenga kuanzisha vikundi 3000 vyenye jumla ya wanavikundi 60,000 kwa
kipindi cha miaka mitatu.
Alisema mradi huo pia
umetoa ajira kwa wakazi wa maeneo ya mradi wapatao 120 ambao kati ya hao 48
wapo wilaya ya Nachingwea ambao wamepata mafunzo ya ukufunzi wa wanavikundi na
sasa wanafanya kazi ya kutoa elimu kwa vikundi katika maeneo yao.
Mama Kikwete alisema, “Vikundi
hivi ni msingi mzuri wa kufanikisha jitihada za kupunguza umaskini wa kipato
kwa wanawake, ni mfumo unaowezesha kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi na
huwavutia watoa huduma za jamii kwani
mtandao wa vikundi hivi unarahisisha kuwafikia wananchi”.
Akisoma ripoti ya vikundi
hivyo Godfrey Makwinya ambaye ni katibu umoja wa walimu alisema madhumuni ya umoja huo ni kuviunganisha
vikundi vya hisa vya wilaya hiyo ili umoja uweze kusimama na kuleta ufanisi
katika vikundi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa
kumbukumbu za fedha kwa wanachama wake na kutatua changamoto zinazowakabili
katika biashara zao.
Makwinya alisema umoja
huo una vikundi 48 ambavyo vimemaliza mzunguko wa mwaka wa kwanza vyenye wanachama
1294 kati ya hao wanaume ni 204 na wanawake 1090. Vikundi vimeweza kujiwekea
akiba ya shilingi 187,842, 650/=, kugawana shilingi 235,653,730/= na kupata faida ya shilingi
47,811,080/=.
Alizitaja changamoto
zinazowakabili kuwa ni kutokuwa na vifa vya kutosha vya kuendesha ofisi vifaa
hivyo ni samani za ofisi na Computer, wanahitaji msaada wa kitaalam ili waweze
kufungua benki yao na uhaba wa fedha za kuendeshea shughuli za umoja wa walimu
wa vikundi.
“Tunahakika kama
malengo yetu yatakuwa kama tulivyopanga
na baadhi ya changamoto zikatatuliwa, utakuwa umepunguza suala la
umaskini kwa kiasi kikubwa kama si
kuondoa kabisa katika wilaya yetu ya Nachingwea”, alisema Makwinya.
Kwa upande wa
wanavikundi vya hisa ambao wamenufaika na mradi huo walimshukuru Mama Kikwete kwa kuanzisha
mradi wa Mwanamke Mwezeshe na kuwapanua akili wanawake walioko vijijini ambao wamekopa fedha na kuzifanyia biashara na hivyo
kujikwamua kiuchumi.
Zuhura Matola alisema, “Nilishindwa
kusomesha watoto kwa kukosa ada, nikaamua kujiunga na vikundi vya hisa baada ya miezi minne ya kuweka akiba nikachukua
mkopo na kuanzisha biashara ya kupika maandazi.
Katika hela ya gawio nimefyatua matofali nataka kujenga nyumba ya kuishi.
“Hela ya gawio iliyobaki
nimenunua vitenge ambavyo naviuza kwa
kuwakopesha watu. Hivi sasa mimi na familia yangu tunakula, tunavaa na wanangu
wanasoma bila ya matatizo hakika mradi huu umetusaidia sisi wanawake ambao
uchumi wetu ulikuwa mdogo tumeweza kufanya mambo yetu wenyewe bila ya kuomba
msaada wa kifedha kutoka sehemu ningine”.
Hadi kufikia mwishoni
mwa mwaka jana mradi wa Mwanamke Mwezeshe ulishaunda vikundi 1,047 na kuwafikia
wanavikundi 26,710 kati ya hivyo vikundi 438 viko wilaya ya Nachingwea na vina wanavikundi 11605.
Miongoni mwa shughuli
za mradi ni kutoa mafunzo ya kuweka akiba ambayo yatawawezesha wanavikundi
kuweka akiba za jumla ya shilingi bilioni moja na nusu kwa kipindi cha miaka
mitatu ya mradi, kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi ulikusanya shilingi
1,518,643,430/= na hivyo kuvuka lengo la mwaka la kukusanya akiba ya shilingi
milioni 500/=.
No comments:
Post a Comment