Tangazo

April 19, 2015

Msama afafanua yanayojiri Kituo cha Honoratha


  Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu taarifa za upotoshwaji zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Honoratha kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu taarifa za upotoshwaji zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Honoratha kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam.

NA LOVENESS BERNARD

MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama, amesikitishwa na taarifa za upotoshaji zilizotolewa hivi karibuni kuhusu kituo cha kulea watoto yatima cha Honoratha kilichopo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Msama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tamasha la Pasaka, amesema kuwa Kituo hicho ni moja ya vituo anavyovihudumia kila mwezi na hakina tatizo la kuwalaza watoto madarasani, kwani wana vyumba kwa ajili ya malazi na kwamba, picha zilizoonyeshwa  zilipigwa watoto hao wakiwa darasani. 

‘’Nimesikitishwa na taarifa hizi, kwani Honoratha ni moja ya vituo ambavyo ninavihudumia, changamoto zao nazifahamu...Kinalea watoto vizuri na baadhi yao wengine tunawasomesha vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini,” alisema Msama.

Aidha, Msama amevitaka vyombo vya habari kuandika habari za ukweli na uhakika ili kuepuka usumbufu  utakaojitokeza kwa wahusika, ikiwamo kwa mlezi na watoto wanaoishi katika kituo hicho ambao walipata adha baada ya taarifa hiyo kutoka.

Alisisitiza kuwa, taarifa hizo hazina ukweli wowote kwani hata mlezi wa kituo hicho hawakufanya mahojiano naye, ikiwamo kumuuliza kwa nini watoto hao walilala darasani mchana huo.

Msama amekuwa akisaidia vituo mbalimbali vya kulea yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kupitia vyanzo vyake mbalimbali ikiwamo mapato yanayotokana na Tamasha la Pasaka.

No comments: