Tangazo

April 17, 2015

VIJANA WA CCM IRINGA WAMPA NGUVU KATIBU WA MKOA HASSAN MTENGA KUKOMBOA JIMBO LA IRINGA MJINI




Mtenga katika kikao na baadhi ya vijana hao.
KIU ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kukomboa jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu inazidi kuongezeka, baada ya umoja wake wa vijana (UVCCM Manispaa ya Iringa) kuahidi kuongeza nguvu ili kuufanikisha mkakati huo.

CCM ililipoteza jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 kwa Mchungaji Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayekaribia kumaliza muda wake.

Katika kikao kilichozikutanisha sekretarieti za umoja huo kutoka katika kata zote 18 za manispaa ya Iringa, Mwenyekiti wa UVCCM wa manispaa hiyo, Kaunda Mwaipyana alisema; “katika kukisaidia chama kushinda uchaguzi huo, kauli mbiu yetu ni chama kwanza mtu baadaye.”

“Tutapita katika matawi na kata zetu zote, tutafanya vikao, mikutano ya hadhara na kuwakumbusha vijana wajibu wa kukipigania chama chao ili mkakati wa kulikomboa jimbo ufanikiwe,” alisema.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga aliwaongezea hamasa vijana hao kwa kuwapa seti 60 za jezi na mipira watakazozitumia kuwahamasisha vijana hao kupitia mchezo wa soka.

“CCM ina vijana wengi sana katika jimbo hili, mnahitaji kukutana na kujipanga, tumieni mbinu zote za kukutana, iwe  vikao, mikutano na hata michezo na ndio maana nimewapa msaada huu,” alisema.

Aliwataka vijana wa chama hicho kujitokeza kwenye vikao visivyo rasmi vya maeneo yao wanayoishi na kuitetea CCM kwasababu majibu ya hoja nyingi za wapinzani wanayo.

Akiwakabidhi jezi hizo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM Mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa alisema  CCM inayo nafasi ya kulikomboa jimbo hilo kama itajipanga vizuri.

“Pamoja na kwamba wapinzani walipata viti 65 katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana, wasisahau kwamba CCM ilipata viti 126; hesabu hiyo inadhihirisha chama chetu kinaungwa mkono mara mbili yao,” alisema.

Aliwataka vijana hao kuweka bendera za chama hicho kila panapostahili katika mitaa yote na akawasihi wasikubali kutumika na kukigawa chama kwa maslai ya wachache.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mahamudu Madenge alisema CCM itaendelea kuwepo hata kama watu wasiotaka kufuata utaratibu wataondoka.

“Wameondoka wengi, wengine hii leo ni viongozi wa vyama vikubwa vya siasa. Pamoja na kuondoka kwao CCM ipo pale pale na inaendelea kupata wanachama,” alisema

No comments: