Tangazo

May 30, 2015

Mtanzania ateuliwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi Shirika la Afya Duniani (WHO)



Dk. Winnie Mpanju-Shumbusho kutoka Tanzania ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Geneva, Uswisi

XXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dk. Margaret F. Chan amemteua Dk. Winnie Mpanju-Shumbusho kutoka Tanzania kuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani, upande wa masuala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na Magonjwa yaliyosahaulika. 

Uteuzi huu umetangazwa rasmi na Dk. Chan wakati wa kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani kilichoanza tarehe 14 hadi 26 Mei, mwaka huu, Geneva nchini Uswisi.

Dk. Mpanju-Shumbusho ni mtaalamu na kiongozi mwenye uzoefu wa miaka zaidi ya 30 katika ngazi za juu za uongozi katika sekta ya Afya na Ushirikiano wa Kimataifa.

Kabla ya uteuzi huu, Dk. Mpanju-Shumbusho alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu Msaidizi ndani ya Shirika la Afya Duniani upande wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na Magonjwa yaliyosahaulika na akiwa na cheo cha Ukurugenzi wa Idara inayoshughulikia Ushirikiano wa Shirika la Afya Duniani na Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund to Fight AIDS, Tuberculosis na Malaria). 

Dk. Mpanju-Shumbusho pia ni mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani kwenye Bodi ya Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria na Bodi mbalimbali za kimataifa.

Hapo awali, Dk. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya kudhibiti Ukimwi na magonjwa mengine katika WHO, Makao Makuu Geneva, Uswisi.

Kabla ya kujiunga WHO, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa East, Central and Southern Africa Health Community Secretariat yenye makao makuu yake, Arusha, Tanzania. 

Vilevile, aliwahi kuwa Mkuu wa Idara na Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Afya ya Jamii na Mgonjwa ya Watoto, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Muhimbili University of Health Science). 

Katika wadhifa huu, Dk. Winnie pia alikuwa mwanzilishi wa mipango mbalimbali ya afya na taaluma na Mshauri Mkuu wa Wizara ya Afya, Tanzania upande wa Afya ya Jamii. Pia amewahi kuwa mjumbe wa Bodi mbalimbali za kimataifa.

Dk. Mpanju-Shumbusho ana Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; vilevile ana Shahada ya Uzamili katika Afya ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Tulane, Marekani na Shahada ya Uzamili katika Medicine (Paediatric and Child Health) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Vilevile ana Shahada ya Uzamifu na Shahada nyingine mbalimbali.

Akiwa Mkurugenzi na Mtaalamu katika Shirika la Afya Duniani, amekuwa mstari wa mbele kuandaa, kuongoza na kutekeleza mipango mkakati ya Dunia ya kujenga na kuimarisha sekta ya afya, hususani katika nchi maskini na zinazoendelea. 

Mipango hii imezaa mafanikio makubwa ikiwamo kujenga uwezo wa nchi maskini kukabiliana na maradhi na afya za kina mama na watoto. 

Sambamba na hilo, mipango hiyo pia ilifanikisha upatikanaji wa dawa za gharama nafuu katika nchi maskini ili kuweza kumudu gharama za matibabu kwa watu maskini. 

Nchini Tanzania, Dk. Mpanju-Shumbusho ameweza kufanikisha upatikanaji wa matibabu na huduma nasaha za kusaidia kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na magonjwa yaliyosahaulika.

Dk. Shumbusho ameolewa na ana watoto wawili, wa kiume na kike.

No comments: