Tangazo

September 18, 2015

KIAMA CHA MAJANGILI CHAJA, BATHAWK YAZINDUA NDEGE MAALUM KUPAMBANA NAO

Ndege aina ya Super Bat DA-50

Na Daniel Mbega, Mkomazi

NI majira ya saa tatu asubuhi Jumatano, Septemba 16, 2015 wakati tunawasili kwenye uwanja mdogo wa ndege (air strip) katika eneo la Kisima ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi inayotenganisha mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.

Uwanja unaonekana mweupe, hakuna ndege! Nikashangaa kwa sababu wenyeji wetu kampuni ya Bathawk Recon wametuambia tunakuja kushuhudia uzinduzi wa ndege maalum zinazopambana na ujangili.

Kilichoonekana mbele yetu ni hema kubwa ambalo mbele yake kulionekana minara midogo iliyosimikwa kama fimbo. Kwenye banda kubwa ikaonekana ndege ndogo aina ya Twin otter. Nikadhani ndiyo inayozinduliwa, lakini Idrisa Jaffary, mwenyei wetu tuliyekuwa naye kwenye gari akasema, hapa siyo hiyo.

Mshangao ukanipata baada ya gari kusimama wakati nilipokiona kifaa mfano wa ndege kikiwa kimeegeshwa kwenye bomba maalum kana kwamba ndege inataka kupaa.

Kama nisingekuwa nazifahamu ndege hizi maarufu kama drones, ningeweza kusema kwamba huo ni mdoli ambao mwanangu angefurahia kama ningempelekea akauchezea.
Kwa siku za karibuni zimekuwa maarufu kwani zinatumika kupeleka misaada mbalimbali hata katika maeneo hatari ya vita ambako hakufikiki kirahisi.

“Hii ndiyo ndege yenyewe,” Idrisa akatueleza. “Hee! Ndiyo hii?” tukajiuliza kwa mshangao. Kwamba Tanzania tumeanza kuitumia teknoloia hii yanaweza kuwa maendeleo mengine mapya.

Mshangao wetu ulimalizika wakati Phil Jones, ofisa mwendeshaji wa mitambo hiyo kutoka kampuni ya MartinUAV ya Marekani iliyotengeneza ndege hiyo aina ya Super Bat DA-50 UAV, alipoanza kutuelezea namna ‘ndege’hiyo (drone) inavyofanya kazi huku akituonyesha kila sehemu na kazi yake.

“Hii ni ndege ambayo haihitaji kuwa na rubani, inaongozwa kwa kompyuta maalum, ina antenna mbili, ina kamera maalum ambazo zinaweza kupiga picha usiku na hata mchana,” akatueleza.
Akasema ndege hiyo ina uwezo wa kuruka urefu wa futi 20,000 kutoka usawa wa bahari na kwenda katika nusu kipenyo cha kilometa 35 kutoka ilipo mitambo ya kuiongoza.
Jones, ambaye baadaye alinieleza kwamba yeye rubani wa zamani wa ndege za kijeshi katika Jeshi la Uingereza aliyestaafu mwaka 2014 ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, akasema ndege hiyo inayorushwa kwa mtindo wa manati (catapult launch system), inaweza kuruka mfululizo kwa muda wa saa 10 ikiwa angani kabla ya kutua na kujazwa mafuta tena.

“Ina mfumo maalum wa kamera ambazo zina uwezo wa kupiga picha hata usiku wa manane na kutambua mienendo ya viumbe wenye damu ya moto kama hayawani na binadamu, hivyo ni rahisi kubaini kama kuna majangili,” akafafanua.

Baada ya maelezo ya takriban nusu saa, hatimaye yeye na wasaidizi wake wakaamua kuirusha ndege hiyo baada ya kuiwasha. Ilichomoka kwa kasi ya ajabu na kuelekea angani ikaanza kuzunguka.

Hapo ndipo tukasogezwa kwenye hema kubwa ambako tuliwakuta wasaidizi wake – Austin Howard na Kory Ferguson – wakiendesha kompyuta hizo na tukashuhudia mazingira halisi ya hifadhi katika eneo husika pamoja na kuona wanyama mbalimbali.

“Sasa hapa unaweza kuona kama kuna wavamizi (majangili) na inakuwa rahisi kuwasiliana na askari wa wanyama pori na kwenda kwenye eneo husika kuwakamata,” anasema Jones.

Hata ilipotua, ilikuja kama ndege za kawaida zinavyokuja, tofauti yake tu yenyewe haina magurudumu. Naam, unaweza kuwa ufumbuzi mwingine wa kupambana na ujangili nchini, tatizo ambalo haliko Tanzania tu, bali katika nchi nyingi barani Afrika.

Taasisi mbalimbali za ndani na nje zikiwemo serikali za mataifa makubwa zimekuwa zikijitahidi kusaidia mapambano hayo kama alivyofanya Rais Barack Obama wa Marekani alipoahidi kutoa Dola milioni 10 (sawa za Shs. 20 bilioni) ili kuimarisha mapambano hayo nchini.

Takwimu zinaonyesha kuwa Bara la Afrika mwaka 1930 lilikuwa na tembo 50 milioni na kwamba hadi kufikia mwaka 2013 tembo waliobakia katika bara zima ni  500,000.

Aidha, takwimu hizo zinaonyesha kwamba katika miaka ya 1960 Tanzania kulikuwa na tembo kati ya 250,000 hadi 300,000 na kwamba wanyama hao walipungua hadi kufikia 130,000 mwaka 2002 na idadi ya tembo hapa nchini imeendelea kupungua kwa kasi ambapo hivi sasa takwimu zinaonyesha kuwa inakadiriwa kuna tembo wasiozidi 55,000.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wastani wa tembo 30 huuawa kijangili kila siku ikiwa ni sawa na tembo 850 kwa mwezina zaidi ya tembo 10,000 wanauawa kila mwaka,hali ambayo inatishia uwepo wa wanyama hao wakubwa zaidi duniani kwa sasa.

Kwenye Hifadhi ya Tarangire, jumla ya tembo 104 waliouawa katika kipindi cha miaka mitatu tu kutoka mwaka 2007 hadi 2009 na katika Hifadhi ya Serengeti idadi ya tembo imepongua kutoka 2,500 mwaka 1985 hadi kufikia 500 mwaka 2012 huku nyati wakipungua kutoka 70,000 hadi 40,000 ujangili huo ukiua faru wengi kutoka 1,000 waliokuwepo mwaka 1985 hadi 20 tu.

Kwenye Pori la Akiba la akiba la Selous inaelezwa kwamba hadi kufikia mwaka 2007 kulikuwa na tembo zaidi ya 70,000 lakini idadi hiyo imeshuka hadi tembo 30,000 tu kufikia mwaka 2012.

Kasi ya ujangili inayoongezeka kila mwaka inachangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo kukua kwa uchumi wa nchi ya China na nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa Asia kama Hong Kong, Vietnam na Philippines.  

Juhudi mbalimbali zimefanywa na wadau wa sekta ya utalii na maliasili, lakini inaoenakana tatizo hilo linazidi kuota mizizi huku taasisi za kimataifa zikiendelea kulipigia kelele bila mafanikio.

Kampuni ya Bathawk Recon Limited ya Tanzania imeitikia kwa vitendo mapambano ya vita dhidi ya ujangili nchini, ambapo leo hii Septemba 16, 2015 ikaamua kuzindua ndege hizo maalum zinazoweza kupambana na ujangili.

 “Haya ni majaribio ya tatu, tulifanya majaribio mara ya kwanza katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa kutumia ndege maalum aina ya DT 16, lakini hayakuonyesha matokeo mazuri,” anasema Michael Chambers, Mkurugenzi wa Mikakati na Mawasiliano wa Bathawk.

Chambers, ambaye amekuwepo nchini Tanzania kwa takriban miaka 20 sasa, anasema jaribio la pili lilifanyika katika Pori la Selous mwezi Mei 2015 kwa kutumia ndege aina ya DT 26 iliyotengenezwa Ufaransa, lakini iliharibika na haikuweza kutoa matokeo mazuri.

Anaibainisha kwamba, katika kipindi cha siku tano cha majaribio tangu Septemba 11, 2015, ndege hiyo mpya aina ya Super Bat DA-50 UAV iliyotengenezwa na kampuni ya MartinUAV ya Marekani, imeonyesha mafanikio makubwa.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi na muasisi wa kampuni hiyo, Tom Lithgow, anasema baada ya majaribio yao kuonyesha mafanikio, sasa wataandaa ripoti yao na kuiwasilisha kwenye taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) pamoja na kwenye Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) ili kama wataridhia, basi waweze kuona namna gani yakuanza utekelezaji kuhakikisha tembo na wanyama wengine wanalindwa.
“Tumefanya kazi kwa ushirikiano na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, hususan Tanapa na Idara ya Wanyamapori, tunaamini baada ya mafanikio haya, nao wataangalia ni kwa namna gani tunaweza kuanza kuitumia,” anasema Tom, Mtanzania ambaye ana uzoefu mkubwa wa mazingira ya porini na utalii kwa ujumla.

Hata hivyo, Mike Chambers anasema, teknolojia hiyo itakuwa ya kwanza kutumia nchini Tanzania katika suala zima la kubaini na kudhibiti ujangili na ni ya gharama nafuu zaidi kwani ndege hizo hazitumii rubani ndani yake, zinatumia mafuta kidogo na kuruka kwa muda mrefu.

“Mbali ya kupambana na ujangili, lakini pia teknolojia hii itasaidia suala zima la uhifadhi kwa kutambua hata idadi ya wanyama waliopo (scouting),” anafafanua Chambers.

Herman van Rooyen na Johnson Makere ni vijana waliohitimu stashahada ya Uhifadhi Wanyamapori katika Chuo cha Wanyamapori cha Mweka mkoani Kilimanjaro, ambao kwa sasa wameelekezwa namna ya kurusha na kuongoza ndege hizo kwa ustadi mkubwa.

Ingawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo maalum na muhimu, lakini wanaielezea teknolojia hiyo kwamba inafaa sana katika suala zima la uhifadhi wanyamapori.

Wanasema, kutokana na tatizo la uhaba wa watumishi na vitendea kazi pamoja na miundombinu duni ndani ya hifadhi na mapori ya akiba, teknolojia hiyo inaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa ikiwa serikali itaikubali na kuitumia.

“Teknolojia hii inasaidia kuwakamata majangili wakiwa wanafanya uharamia wao ndani ya hifadhi na hivyo kuondoa malalamiko yaliyopo sasa kwamba majangili wanaokamatwa wanakuwa wanasingiziwa,” anasema Makere.

Makere anaongeza: “Hivi sasa utaratibu unaotumiwa ni kama wa mbwa kufuata nyayo na harufu kwani majangili mara nyingi wanakuwa wanakamatwa wakiwa majumbani mwao, lakini hapa watakamatwa humo ndani na hivyo kuukazia ushahidi kwani picha zipo na watakuwa na vidhibiti.”

Kampuni ya Bathawk Recon inajipambanua kwamba kwa kuja na teknolojia hiyo ya utambuzi inaweza kuwa suluhu ya janga la ujangili kwa kuwa inao uwezo wa kutambua majangili hata kama wakijificha, labda kama watachimbia ardhini.

“Na kama watajichimbia basi itakuwa faida zaidi, kwa sababu hawawezi kufanya lolote bila kuonekana,” anaongeza Jones, ambaye kwa zaidi ya miaka 10 amekuwa rubani wa ndege za kivita kwenye Jeshi la Kifalme (Royal Armed Forces).

Ofisa uhifadhi kutoka Hifadhi ya Tarangire, Marandu, ambaye alimwakilisha Mhifadhi katika uzinduzi huo, anasema anaamini teknolojia hiyo ni nzuri na inaweza kusaidia kuwahifadhi wanyama.
“Katika mapambano dhidi ya ujangili na ustawi wa maliasili, mbinu yoyote yenye kuleta matokeo chanya ni vizuri ikapokelewa na kujaribiwa, kama inafaa basi itakuwa msaada mkubwa kwa taifa,” anasema.

Sera ya Taifa ya Wanyamapori ya mwaka 1998 inaelekeza kuwa aina zote za viumbe hai zihifadhiwe, wanyamapori wasitumiwe kiasi cha kuifanya idadi yao ipungue na kuwa katika hatari ya kutoweka na kuhakikisha Taifa linaendelea kumiliki wanyamapori na kusimamia kwa niaba ya wananchi.

Ndege zilizojaribiwa

DT-18 ilijaribiwa Tarangire

Hii ilitengenezwa Ufaransa. Ni ndogo sana, inaweza kuruka kwa saa mbili tu katika nusu kipenyo cha kilometa 15 kutoka ilipo mitambo.

DT-26 ilijaribiwa Selous

Imetengenezwa Ufaransa na kampuni ya Delair Tech. Hii ni kubwa kidogo, ina uwezo mkubwa na inatumia viwango vya satelaiti za kijeshi vya mawasiliano kutumana kupokeataarifa pamoja na namna ya kuongozwa kwake.

Superbat DA 50 – Imejaribiwa Mkomazi

Imetengenezwa Marekani na kampuni ya MartinUAV. Inaitwa MLB Super-Bat DA-50. Inatumia injini yenye mapigo mawili na uwezo wa 50cc ikiwa na genereta la Watts 75 pamoja na mafuta. Urefu wake ni futi 8.5 x 5.3 x 2.25 inapokuwa imeunganishwa, lakini ikiwa bado haijaungwa ina urefu wa futi 3.5 x 1.25 x 1.5. Kasi yake ni kati ya 40 hadi 70kts, inakaa angani kwa saa 10 mfululizona inaruka kimo cha futi 15,000 hadi 20,000 bila kupoteza mawasiliano.


0656-331974

No comments: