Tangazo

October 24, 2015

MAGUFULI AFUNIKA JIJI LA DAR

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli akihutubia mkutano wa kufunga kampeni katika mkoa wa Dar es Salaam leo, kwenye viwanja vya Jangwani.
UMATI wa wananchi uliofurika kwenye viwanja vya Jangwani leo
RAIS Jakaya Kikwete akimtambulisha Dk Magufuli kwa wananchi
RAIS Jakaya Kikwete akikumbatiana na Dk Magufuli
Na Rashid Zahor RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Jakaya Kikwete, amesema mgombea urais aliyesimamishwa na chama hicho, Dk. John Magufuli, kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka huu, ameshashinda na kwamba anachosubiri ni kuwa rais. 

 Amesema kwa kawaida nyota njema huonekana asubuhi, hivyo sio siri kwamba Dk. Magufuli atakuwa rais wa awamu ya tano wa Tanzania na kusisitiza kuwa, wagombea wengine wa nafasi hiyo ni marais vivuli. 

 Rais Kikwete alisema hayo leo, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni wa kumnadi Dk. Magufuli, uliofanyika kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salalaam. 

 Mkutano huo ulikuwa wa mwisho kwa Dk. Magufuli katika Jiji la Dar es Salaam, baada ya kutembelea majimbo yote 10 ya mkoa huo kwa ajili ya kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuomba kura kwa wananchi. "Nilidhani baada ya (mgombea) kupita katika wilaya na majimbo yote ya Dar es Salaam, mkutano wa leo ungehudhuriwa na watu wachache, kumbe wamekuwa wengi zaidi. nyota njema huonekana asubuhi, Magufuli umeshashinda, ndiye rais wa awamu ya tano, marais wengine ni vivuli,"alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika kwenye viwanja hivyo. 

Alimpongeza Dk. Magufuli kwa kuweza kuzunguka nchi nzima kwa gari kufanya kampeni, badala ya kupanda helkopta na kuwaponda wagombea wengine waliotumia usafiri huo wa anga, lakini walishindwa kuhutubia mikutano yao. 

 Rais Kikwete alisema mgombea aliyepanda gari aliweza kuhutubia mikutano yake na kunadi sera za CCM kwa saa nzima katika kila mkutano wakati wagombea wengine waliwataka wananchi wazisome sera zao kwenye tovuti za vyama vyao. 

 Alisema kutokana na kutembelea mikoa yote 31 ya Tanzania, Dk. Magufuli amepata nafasi nzuri ya kuijua nchi ilivyo, hivyo amewaomba wananchi wampigie kura nyingi ili awe rais wao. 

 Baada ya kusema maneno hayo, Rais Kikwete aliwauliza wananchi iwapo watamchagua Dk. Magufuli kuwa rais, nao wakamjibu 'ameshapata'. 

Rais Kikwete aliuliza tena swali hilo huku akitazama pande zote za uwanja na kuhakikishiwa kuwa ameshapata. Majibu hayo ya wananchi yalikwenda sambamba na mayowe ya 'rais, rais, rais.' Rais Kikwete alimwelezea Dk. Magufuli kuwa anatosha kuwa rais na kwamba hakuna mgombea wa kumfananisha naye, miongoni mwa wagombea wanane wanaogombea nafasi hiyo. "Mwaka 2005 nilitembea kilometa 32,000 kwa gari kuomba kura nchi nzima. Nilipomaliza nilikuwa hoi. Nampongeza Dk. Magufuli aliyetembea umbali wa kilometa zaidi ya 45,000, lakini bado yuko fiti,"alisema Rais Kikwete.

 Alisema anamuomba Dk. Magufuli achaguliwe kwa kura nyingi kuwa rais keshokutwa, ili mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan, awe makamu wa rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania. 

 "CCM haikukosea kumteua Magufuli, amekamilika, mtu wa watu, tunawajua wanaowafaa wananchi na kuifaa Tanzania kwa sababu tunawajua,"alisema Rais Kikwete na kuamsha shangwe kutoka kwa wananchi. 

 Akizungumzia kauli za mwasisi wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, aliyejitoa katika Chama hivi karibuni, Rais Kikwete alisema hakuwaeleza ukweli wananchi kwa vile alikuwa na mgombea wake, ambaye jina lake lilikatwa mapema. "Huyu mzee amedai kuwa CCM inaendeshwa vibaya, mchakato wa kumteua mgombea urais ulifanyika vibaya, hataki kusema ukweli. 

Aliyemtaka hakupata,"alisema Rais Kikwete na kuwafanya wananchi wamshangilie. Alisema utaratibu wa kumpata mgombea rais uliotumiwa na CCM mwaka huu, ndio uleule uliotumika mwaka 1995 na 2005, ambapo naye alikuwa miongoni mwa makada waliojitokeza kuwania nafasi hiyo. 

 Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa katiba ya CCM, Kamati Kuu inatakiwa kupeleka mbele ya Halmashauri Kuu majina matano kabla ya kuchujwa na kupelekwa matatu kwenye kikao cha mkutano mkuu. 

 Alisema mwaka 1995, wagombea walikuwa 17, lakini waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM ni Jaji Joseph Warioba, Jaji Mark  Bomani, Pius Msekwa, Cleopa Msuya, Benjamin Mkapa na yeye. Katika uteuzi huo, Mkapa aliteuliwa kuwa mgombea urais. 

 Aidha, alisema katika uchaguzi wa mwaka 2005, hakukuwa na mabadiliko yoyote na kwamba, utaratibu uliotumika ni ule ule, ambapo wagombea walikuwa 11, lakini waliopitishwa walikuwa Kikwete, Msuya, Mark Mwandosya, Abdalla Kigoda na Fredrick Sumaye. "Miaka yote hiyo Mzee Kingunge alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, lakini analalamika kwamba mwenyekiti alikuwa na jina lake mfukoni. 

Ina maana Mzee Mkapa naye alikuwa na jina lake mfukoni?" Alihoji. "Kingunge alimpenda mtu, ambaye kichama hakukidhi vigezo vyake. Huu ni uzee,"alisema Rais Kikwete na kuwahoji wananchi 'nani kama Magufuli' na kujibiwa kwa mayowe kwamba hakuna. 

 Alisema hana wasiwasi kwamba keshokutwa wananchi watajitokeza kwa wingi kupigakura na kwamba ipo sura ya ushindani, lakini kwa Magufuli hakuna wa kushindana naye. 

 Alimwelezea Dk. Magufuli kuwa ni mwadilifu, mkweli na amekuwa akitoa kauli zake bila kumung'unya maneno na kuahidi kupambana na rushwa na ufisaidi. 

 Rais Kikwete alisema wapinzani wamekuwa wakipatwa na kigugumizi kuzungumzia rushwa na ufisadi kwa vile wanaishi na mambo hayo na kuongeza kuwa, mgombea wa upinzani (Edward Lowassa), hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa vile rushwa itastawi. Aidha, alimwelezea Dk. Magufuli kuwa ni mpenda watu, mtu wa watu, mchapakazi asiye na mfano na anayependa kuona mambo yake yanakwenda vizuri. 

Pia alimwelezea kuwa ni mtu anayependa kukagua miradi anayoisimamia ili mambo yaende vizuri. "Anakereketwa kuona Watanzania bado wanyonge, anawapenda vijana, anaguswa na changamoto zinazowakabili na ameahidi kuzitafutia ufumbuzi,"alisema. 

 Rais Kikwete alisema miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Dk. Magufuli na ambazo anaamini atazifanyiekazi ni pamoja na kuboresha maisha ya walimu, kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya juu wanapata mikopo na vijana wanapata ajira. 

 Aliitaja ahadi nyingine ya Magufuli, ambaye itaweza kuleta ahueni kwa Watanzania kuwa ni pamoja na kutoa fursa za mikopo kwa vijana na kinamama, kutambua na kuthamini nafasi ya wafanyabiashara.

 "Wapo baadhi ya watu wanawatisha wafanyabiashara, hao wanataka hela zetu, msibabaike. Hawezi kutaka viwanda halafu akawachukia wafanyabiashara. Huyu ndiye Magufuli ninayemjua mimi na hata CCM inamjua na ikampitisha,"alisema. 

 Rais Kikwete pia alimwelezea Dk. Magufuli kuwa ni mgombea pekee aliyetoa ahadi ya kutetea nafasi za wanawake katika haki ya ajira, elimu, uongozi, ardhi na malipo sawa kwa jasho lao, tofauti na wagombea wa vyama vingine.

 "Magufuli ameahidi kuongeza mchango wa serikali kwenye Benki ya Wanawake, hivi kinamama mnahitaji mtu mwingine wa aina gani?" Alihoji Rais Kikwete. "Hivi ni kweli mtu wa aina hiyo unamnyima kura, umpe nani? Hakuna (mgombea) aliyewazungumzia walemavu kama Magufuli,"aliongeza.

 Rais Kikwete pia alimwelezea Magufuli kuwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kuendeleza jitihada za kuinua michezo nchini, zilizoanzishwa na serikali ya awamu ya nne ili iweze kufika matawi ya juu zaidi. "Nimejitahidi kuinua michezo, nilipofikia panahitaji tingatinga kututoa tulipo, twende kucheza kombe la Afrika na Dunia,"alisema Rais Kikwete.

 Mwenyekiti huyo wa CCM pia aliwatambulisha wagombea wote wa ubunge katika majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam na kuwaombea kura wa wananchi. Wagombea hao ni Iddi Azzan (Kinondoni), Didas Masaburi (Ubungo), Dk. Fennela Mukangara (Kibamba), Kippi Warioba (Kawe), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Jerry Silaa (Ukonga), Bona Karuwa (Segerea), Abbas Mtemvu (Temeke), Dk. Faustine Ndugulile (Kigamboni), Murtaza Mangungu (Mbagala).  
Baada ya utambulisho huo, Rais Kikwete aliwataka wananchi kuwachagua wagombea wa CCM ili wasaidie jitihada za serikali za kuwaletea maendeleo, badala ya wagombea wanaoendekeza maandamano na kususia vikao vya bunge. "Jumapili nendeni kwa wingi na mapema mkapigekura.

 Amani itakuwepo, hapatatokea chochote. Bahati nzuri waliokwenda mahakamani wameshindwa. Mahakama imethibitisha kwamba kituo cha kupigia kura si mahali pa mikutano, ni marufuku,"alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa. "Hatumnyimi mtu haki yake, tunachotaka ni amani, wananchi wachague viongozi wanaowataka kwa uhuru,"alisisitiza. 

 Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Magufuli aliyeanza kuhutubia saa 10.37 jioni, aliahidi kupambana na mafisadi na wala rushwa na pia kukwamua wananchi kutoka katika hali duni na umasikini. Dk. Magufuli pia aliahidi kuwanyang'anya wafanyabiashara walioshindwa kuviendeleza viwanda walivyovinunua ili wapewe watu wengine, watakaokuwa na uwezo wa kuviendeleza.

 "Wanaovimiliki waviendeleze, bila hivyo tutavitaifisha wapewe wengine kuviendeleza ili vitoe ajira,"alisiema. Alisema serikali yake itaanzisha viwanda vingi nchini na kwamba atakuwa rafiki wa aina zote za wafanyabiashara kwa vile ni watu muhimu katika kutoa ajira. Dk. Magufuli alijikuta akimwinua kitini Rais Kikwete pale alipowakosoa Mawaziri Wakuu wa zamani, Sumaye na Lowassa kwa kudai kuwa serikali haijafanya lolote, wakati walikuwa na nafasi kubwa serikali na pia wasaidizi wa rais. 

 Huku akimuomba radhi Rais Kikwete, alisema Lowassa hakuweza kumsaidia lolote, kauli iliyomfanya ashangiliwe na wananchi huku Rais Kikwete akienda kumpongeza na kumtaka aendelee kuzungumza ukweli. Dk. Magufuli pia alielezea mikakati mbalimbali ya serikali ya kuboresha ujenzi wa barabara za Dar es Salaa, zikiwemo zile za juu (flyovers), ambazo alisema zitabadili sura ya Jiji na kulifanya lionekane la aina yake.

 Pia aliwashukuru viongozi wa zamani wa Chama na serikali kwa kumuombea kura kwa wananchi na kusema kuwa, hiyo ni baraka kubwa kwake, inayomfanya awe na uhakika mkubwa wa kuchaguliwa kuwa rais. 

 Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Mawaziri wakuu wastaafu, Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro.

 Msafara wa Dk. Magufuli uliwasili kwenye viwanja hivyo saa 9.19 huku akiwa amesimama kwenye gari na kupunga mikoni kwa wananchi waliokuwa wakimshangilia kwa kuimba rais, rais, rais'. 

 Rais Kikwete aliwasili uwanjani hapo saa 9.30 na kupokewa na viongozi waliomtangulia huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kuliko mikutano yote iliyofanyika hivi karibuni kwenye viwanja hivyo. Akisoma risala ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM mkoa, Ramadhani Madabida, alimuhakikishia Dk. Magufuli kuwa watampa kura nyingi ili awe rais wa awamu ya tano.

No comments: