Tangazo

October 2, 2015

WAIMBAJI TAMASHA LA AMANI KUANZA KUWASILI IJUMAA

Mwenyekiti wa Tamasha la Kuombea Amani, Alex Msama akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 4 kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Hamisi Pembe. (Picha na Francis Dande)
Na Mwandishi Wetu

WAIMBAJI watakaoshiriki katika tamasha la kuombea Amani Uchaguzi Mkuu 2015 wanaanza kuwasili Ijumaa Oktoba 3.

Aklizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa tamasha hilo, Alex Msama amesema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika kwa asilimia 100 huku waimbaji kutoka nje ya nchi wanatarajiwa kuwasili kuanza Ijumaa.

Aliwataja waimbaji hao kuwa ni Sipho Makhabane, Solly Mahalangu (Afrika Kusini), Ephraim Sekereti (Zambia), Solomon Mukubwa (DR Congo), Sarah K (Kenya).

Aidha kutakuwa na waimbaji wadhawa akiwemo malkia wa muziki wa injili Afrika Mashariki na Kati, Rose Muhando, Upendo Nkone, Jesca BM, Bonny Mwaitege, Christopher Mwangira, John Lissu.

Kwa upande wa kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama, Kweaya ya AIC Chang'ombe na Kwaya ya St. Adrew Aglikana ya Dodoma.

Wakati huohuo Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limeipongeza Kampuni ya Msama Promotions kwa kuwa wabunifu wa kuinua vipaji vya waimbaji wa muziki wa Injili Tanzania ambao wanapata nafasi ya kutambulika kimataifa.

Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, alisema kuwa ufanikishaji huo wa kazi za waimbaji inayofanywa na Msama ni baada ya kukamilisha taratibu zote ikiwemo ufuatiliaji wa vibali vya kufanikisha tukio hilo la kuombea amani Oktoba 4.

Mngereza alisema tamasha hilo ni lenye maana kubwa kutokana na maudhui yake, hasa ikizingatiwa nchi inakabiliwa na Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 25.

Alisema tamasha hilo linasisitiza kuwa amani ni kitu cha msingi hasa kwa masuala ya kisiasa na kiuchumi, ambavyo havitapata mwelekeo wake iwapo amani hiyo ikikosekana.

“Kama hakuna amani vitu vyote havifanyiki, tamasha hilo limekuja wakati muafaka kwamba sisi ni wamoja, Watanzania tuzingatie misingi ya amani.

“Tumekuwa ndugu bila kubaguana kwa hali yoyote, amani tuliyopewa na Mungu, tuileee na kuitunza tunu hiyo kwa sababu ndiyo chachu ya maendeleo yetu na taifa kwa ujumla,” alisema.

Mkurugenzi wa Msama Prmotions, Alex Msama alisema maandalizi ya kuelekea tamasha hilo yamekamilika kwa kiasi kikubwa, hivyo alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kufanikisha tamasha hilo.

“Nawasihi wapenzi na mashabiki wa muziki wa Injili na wengine wenye mapenzi mema kwa nchi yao, wajitokeze kwa wingi katika Uwanja wa Taifa katika tamasha la kuombea amani Uchaguzi Mkuu,” alisema Msama.

Aidha, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kukubali kubeba jahazi la tamasha hilo, kwa kukubali kuwa mgeni rasmi ambapo atatumia tukio hilo kuwaaga mashabiki wa muziki wa Injili.

No comments: