Tangazo

February 22, 2016

“WATANZANIA WAZINGATIE SHERIA ZA MTANDAO, KIFUNGO NI MIAKA 30 AU ZAIDI” – KITWANGA

Charles KitwangaWaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga (pichani) amewataka Watanzania kuzingatia sheria za mtandao ambazo zilitungwa mwaka jana kufuatia kuonekana kuwepo kwa baadhi ya watumiaji ambao wamekuwa hawafati sheria.

Mhe. Kitwanga alisema wanaotumia mtandao wanawajibu wa kutumia mtandao kwa matumizi ambayo hayatavunja sheria na ambao watakuwa wakikiuka sheria hiyo serikali haitawavumilia na watawachukulia hatua za kisheria.
Advera Bulimba
Msemaji wa Jeshi la Polisi Advera John Bulimba.
“Adhabu ya kuvunja sheria hii ya makosa ya mtandao ni mbaya sana na ninataka kuwambia Watanzania wazingatie sheria za mtandao … kifungo ni miaka 30 au hata zaidi,” alisema Kitwanga.

Aidha aliwataka ambao wamekuwa wakitukanwa katika mitandao ya kijamii wapeleke malalamiko Polisi na serikali imejipanga kuwachukulia hatua watumiaji ambao wamekuwa hawafati sheria za mtandao.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba alisema kuwa jeshi hilo limekuwa likiwachukulia hatua watumiaji wote wa mitandao ambao wamekuwa wakikutwa na hatia ya kufanya matumizi mabaya.

Alisema tangu imetungwa sheria hiyo wameshafungwa baadhi ya watumiaji na kesi saba zikiwa mahakamani na bado wanaendelea kufatilia watumiaji wengine ili wawachukulie hatua.
“Polisi tunaendelea kuwachukulia hatua watumiaji ambao wanakuwa na makosa na kwasasa kuna kesi saba zipo mahakamani … tangu sheria imetungwa kesi tunazopokea zinazohusu mitandao zimepungua kutoka 25 hadi 30 kwa siku ila siku hizi zinakuwa 10 au chini ya hapo,” alisema Bulinda.

Nae mmoja wa watumiaji wa mtandao, Grace Mwanga aliwashauri Watanzania wenzake kudumisha maadili ya kitanzania na kuifanya mitandao kama njia ya mawasiliano kama jinsi lilivyo kusudiwa na waanzilishi wa mitandao hiyo.

“Watanzania tudumishe maadili yetu ya zamani, mitandao isitufanye tusahau asili yetu … tutumie mitandao kuwasiliana na hata kufanya matangazo ya biashara zetu,” alisema Grace.

No comments: