Tangazo

April 25, 2016

Bodi ya Mikopo, TAHLISO wakubaliana kuendeleza ushirikiano

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Jerry Sabi akiongea na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa TAHLISO Bw. Stanslaus Kadugalize. Picha na HESLB. 
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) kutoka Chuo Kikuu cha Bugando Bw. Elia Kandonga akiongea katika mkutano kati ya TAHLISO na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na kufanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki. Picha na HESLB
·   Naibu Waziri awakumbusha wanufaika kurejesha mikopo
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Viongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) wamekutana mjini Dodoma mwishoni mwa wiki ili kubadilishana mawazo na kukubaliana kuendeleza ushirikiano ili kutatua kero za wanafunzi.
Katika mkutano huo, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAHLISO kutoka taasisi za elimu ya juu nchini wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw. Peter Kadugalize walikutana kwa siku nzima na viongozi wa HESLB walioongozwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi na kujadiliana njia bora za kutatua kero za wanafunzi.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Kadugalize aliiomba HESLB kuhakikisha Mameneja wa kanda wa HESLB waliopo katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya na Zanzibar wanatembelea vyuo vilivyopo katika maeneo yao na kukutana na viongzi wa Serikali za wanafunzi kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao.
"Tunaomba hawa Mameneja wa Kanda washirikiane nasi kwa kuja vyuoni na kukutana na sisi...kero nyingi za wanafunzi zinaweza kutatuliwa kwa njia hiyo badala na kurundikana hadi tukutane na viongozi wa wakuu wa Dar es Salaam," alisema Bw. Kadugalize.
Kuhusu changamoto zinazowakabili vyuoni, Bw. Kadugalize alizitaja baadhi ya kero kuwa ni pamoja uelewa mdogo wa baadhi ya wanafunzi kuhusu sifa za kupata mikopo inayotolewa na HESLB hususan wale wanaokata rufaa baada ya kukosa katika maombi yao ya kawaida.
Akizungumzia katika mkutano huo, Bw. Sabi, ambaye aliteuliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufunzi mwezi Februari mwaka huu kushika nafasi hiyo, alisema ushirikiano katika ya HESLB na TAHLISO ni muhimu na kuahidi kuuendeleza.
"Ushirikiano huu ni muhimu, ndiyo maana tumekubali mimi na timu yangu kuja kuwasilikiza na kuwapa majibu ya maswali yenu," aisema Bw. Sabi.
Akifafanua kuhusu sifa za waombaji mikopo, Bw. Sabi alisema sifa na vigezo hutolewa kila mwaka na kuwasihi waombaji wote wa mikopo kusoma kwa makini na kuzingatia sifa hizo kabla ya kuomba mikopo.
"Ninawasihi msome kwa makini sifa na vigezo kabla ya kuomba...kuhusu rufaa, ni muhimu kila mwombaji anayekata rufaa kuthibitisha uhitaji wake kwa kuaambatanisha nyaraka muhimu zinazohitajika na ambazo zimethibitishwa na mamlaka husika...bila hivyo sisi tutashindwa kuthibitisha," alisema Bw. Sabi katika mkutano huo.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi,, Teknolojia na Ufunzi Mhandisi Stella Manyanya amewataka wahitimu wa vyuo vikuu ambao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na HESLB kuhakikisha warejesha mikopo hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wahitimu wa mwaka 2015 kutoka katika taasisi za elimu ya juu nchini waliofanya vizuri katika masomo yao iliyoandaliwana TAHLISO, Naibu Waziri watanzania wengi wanahitaji mikopo ya elimu ya elimu ya juu na hivyo ni muhimu fedha hizo zikarejeshwa ili ziwanufaishe wengine.
"Kuna wengi wanaohitaji na bajeti ni finyu, ni vema mkarejesha ili ziwanufaishe wengine...na wazazi wahakikishe vijana wao waliopata elimu kwa nia ya mikopo wanaanza kurejesha," alisema Naibu Waziri katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mt. Gaspar mjini Dodoma mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na watendaji kutoka HESLB, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), wazazi na wanafunzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Jerry Sabi alisema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, jumla ya shilingi 2.3 trilioni zilikuwa zimetolewa kama mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na kuwa Bodi imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ili kurejesha mikopo iliyoiva.
Mikakati hiyo ni pamoja na kuwashirikiasha watendaji wakuu wa serikali wakiwemo Katibu Mkuu - Hazina na Msajili wa Hazina ambao wamewaelekeza waajiri wote serikalini kuihakikisha wanufaika wote wa mikopo wanarejesha mikopo.
Makakati mwingine ni kuingia mkataba na Kampuni ya CreditInfo Tanzania Ltd ambao utaziwezesha taasisi za fedha nchini kuwabaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya ju kabla ya kuwakopesha pale wanapokwenda katika taasisi hizo kwa ajili ya kukopa fedha.

HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 kwa lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi watanzania wahitaji waliopata nafasi ya kusoma katika vyuo vikuu. Aidha, HESLB ina jukumu la kukusanya madeni yote ya mikopo ya elimu ya juu iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.

No comments: