Tangazo

November 22, 2016

UNDP, ESRF wafanya uzindua Ripoti ya Maendeleo Afrika 2016

 Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida akitoa neno la ufunguzi katika halfa ya uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016.
 Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Awa Dabo akizungumza kwa niaba ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika halfa ya  uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016.
 Mgeni rasmi katika halfa ya uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga akitoa hotuba kwa niaba ya serikali na kueleza mikakati ambayo wameipanga ili kuweka usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume pamoja na kuwawezesha wanawake ili waweze kushirki katika shughuli za maendeleo.
 Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria halfa hiyo
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga akikata utepe kuashirikia kuzinduliwa kwa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016.
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida (wa  kwanza kushoto), Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Awa Dabo (wa tatu kulia), Mkuu wa Kitengo cha Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Timothy Mgonja na Mwakilishi wa UN Women wakionyesha kitabu cha Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016.
 Wageni rasmi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya halfa ya uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016.

Na Mwandishi Wetu
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) likishirkiana na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) limefanya uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2016 ambayo imekuwa na kauli mbiu ya Kuongeza Kasi ya Kuweka Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Wanawake.

Akizungumza kwa niaba ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Awa Dabo alisema kuwa ripoti hiyo inaonyesha jinsi gani watu wanaoishi Afrika wanapiga hatua kupata maendeleo lakini wakikabiliwa na changamoto usawa wa kijinsia na uwezeshaji kwa wanawake.

"Kupitia ripoti hii UNDP inaonyesha jinsi gani watu wanaoishi Afrika wanajihusisha na shughuli za maendeleo lakini bado kuna changamoto ya usawa wa kijinsia, jambo la kijisnia linagusa kila sehemu kuanzia serikalini, taasisi za kijamii, mashirika binafsi na hata kwenye vyombo vya habari,

"Kwa sasa Afrika ndiyo ya mwisho kwa maendeleo ya binadamu kulinganisha na sehemu zingine duniani na jambo la usawa wa kijinsia linabaki kuwa muhimu, UNDP itaendelea kushirikiana na serikali kusaidia kupatikana usawa wa kijinsia na uwezeshaji kwa wanawake ili kumaliza vitendo hivi ambavyo vinachangia Afrika kuwa nyuma kimaendeleo," alisema Dabo.

Nae mgeni rasmi katika uzinduzi wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga alisema serikali inafahamu kuwepo kwa changamoto hiyo na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwepo kuwapa nafasi za uongozi wanawake.

Alisema ripoti hiyo itaisaidia Serikali kuweza kuweka mikakati bora na ambayo itaweza kumaliza tatizo la usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuangalia kwa jinsi gani watawawezesha wanawake ili waweze kujihusisha na shughuli za maendeleo ambazo ziwasaidia kukuza kipato chao lakini pia taifa kwa ujumla.

"Ripoti hii itasaidia kupata mipango ambayo inaweza kutumiwa kwa ajili ya changamoto iliyopo ya usawa wa kijinsia, ripoti inaonyesha jinsi gani wanawake wanaweza kusaidia kuleta maendeleo lakini bado wanakabiliwa na tatizo la usawa na hivyo kukwamisha ukuaji wa uchumi,

"Naomba niwahakikishie serikali ya Tanzania itakwenda kuitumia ripoti kuboresha sera, mipango na vitendo ili kupatikana usawa wa kijinsia na pia kusaidia kukuza uwezeshaji kwa wanawake wa Tanzania, serikali imekuwa ikisaidia kuweka usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na hata makamu wetu wa Rais ni mwanamke na katika hili tutahakikisha wanawake wanaendelea kupata nafasi na kusaidia kuleta maendeleo," alisema Nkinga.

Kwa upande wa ESRF kupitia Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Tausi Kida alisema "Tunafahamu kuwa usawa wa kijinsia ni jambo ambalo limekuwa likitafutiwa ufumbuzi tangu tukipata uhuru na katika hilo (ESRF) tumekuwa tukiunga mkono jitihada za serikali kwa ajili ya kuweka usawa kwa Watanzania, tunaamini ripoti itasaidia kuleta maendeleo kwa Tanzania katika mpango wa maendeleo ulizindiliwa Dodoma"

No comments: