Tangazo

November 3, 2014

MSAMA AMPONGEZA JK UJENZI WA KIDONGO CHEKUNDU DAR

 Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akitoa pongezi kwa Rais Jakaya Kikwete baada ya kuzindua Kituo cha Michezo cha Kidongo Chekundu.


Na Francis Dande

MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuzindua Kituo cha Kisasa cha Mafunzo ya michezo eneo la wazi la Kidongo Chekundu, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi wa Kituo hicho uliofanyika leo, Msama alisema Kituo hicho kitasaidia kuzalisha vijana wengi wenye vipaji na kuandaliwa vizuri.

Hicho ni Kituo kinachojengwa kwa udhamini wa kampuni ya Symbion ikishirikiana na Klabu ya Sunderland ya Uingereza kwa lengo la kuinua kiwango cha sekta hiyo kitaifa na kimataifa. 

Msama ambaye ni mdau wa tasnia ya burudani kupitia uratibu wa matamasha ya muziki wa injili ya Pasaka na Krismas, alisema kituo hicho kitakuwa mwanzo mpya wa kuimarika kwa sekta hiyo. 

Alisema, akiwa mdau wa maendeleo ya vipaji vya aina mbambali, anaiona fursa zilizopo kupitia kituo hicho ambacho baada ya kukamilika, kitasaidia vijana wenye vipaji kufikia malengo kwa maslahi yao binafsi na michezo.

Msama alisema kwa upande wa soka, anaamini kituo hicho kilichozinduliwa
na Rais Kikwete, kitakuwa chachu ya vipaji ambavyo nitakuwa msaada kwa timu nyingi nchini na hatimaye timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.

“Nampongeza Rais Kikwete kuzindua Kituo hiki ambacho naamini kitasaidia maendeleo ya michezo nchini  kwa kuibua na kukuza vipaji vya vijana ambao watakuwa msaada mkubwa kwa taifa,” alisema Msama.

Alisema watanzania wana kila sababu ya kumpongeza Rais Kikwete ambaye ataondoka madarakani mwakani baada ya miaka yake 10 ya uwepo wake  madarakani akiwaachia Kituo hicho ambacho kitabaki kama alama yake.

“Ujenzi wa kituo hiki kilichozinduliwa na Rais Kikwete, ni habari njema kwa wadau wa michezo na burudani, kunafungua fursa kwa vipaji vipya kuibuliwa na kuendelezwa kwa maslahi yao  na taifa,” alisema Msama.

Alisema japo kituo hicho kinajengwa kwa malengo ya kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo, anaamini kama kitakuwa na uwanja wa kutosha, hata wao Msama Promotions ambao ni wadau wa matamasha ya injili, watapata fursa ya kuendesha matukio yao.

Msama Promotions, ndio waasisi wa matukio ya muziki wa injili kupitia matamasha ya Pasaka na Krismas ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki huo wa kuutangaza ukuu wa Mungu tangu mwaka 2000.

Matukio hayo mawili yamekuwa chachu ya kukua kwa muziki wa injili kwani yamekuwa yakishirikisha waimbaji mahuiri wa ndani na nje ya nchi ikiwemo kutoka Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na Burundi.

No comments: