Tangazo

December 21, 2016

MACHINJIO YA KISASA YA SUNGURA KUJENGWA NCHINI

Mkurugenzi wa Kampuni ya Rabbit Republic ambaye ni mfugaji wa sungura kutoka Kenya, Moses Mutua (kulia) akielezea mipango yake ya kuzanzisha machinjio ya kisasa ya sungura hapa nchini, wakati wa hafla ya Kampuni ya Namaingo kugawa sungura kwa  vikundi 20 vya wajasiriamali, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. 
Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Donald Bombo,Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo, Ubwa Ibrahim na Meneja wa Mradi wa Sungura, Amos Misinde. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA)


Na Richard Mwaikenda;Kamanda wa Matukio Blog

WAKATI Tanzania ikijielekeza katika uchumi wa viwanda, mpango wa ujenzi wa machinjio ya kisasa ya sungura yatakayogharimu sh. milioni 100 utaanza mapema mwakani, ukiratibiwa na Kampuni ya Rabbit Republic.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Moses Mutua alisema hayo wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa miradi ya sungura kwa wajasiriamali uliofanywa na Kampuni ya Namaingo Business Agency jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Mutua ambaye ni mfugaji wa sungura kutoka nchini Kenya, alisema uamuzi wa kujenga machinjio ya sungura  unatokana na kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kufuga sungura.

Alisema awali, mradi huo ulihusisha kusafirisha sungura hai hadi Kenya, lakini ongezeko la watu wanaohitaji kujishughulisha na biashara hiyo limesababisha kuwapo haja ya kujenga machinjio hayo.

Alisema nia na uthubutu wa serikali ya Rais John
Magufuli kuwaondoa wananchi wanyonge katika umasikini, ni miongoni mwa mambo yaliyomsukuma kufikia uamuzi huo.

"Machinjio hayo yatakayojengwa Dar es Salaam
yatakuwa na uwezo wa kuchinja sungura wengi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kutenganisha vizuri ngozi, nyama na kucha," alisema.

Alisema bidhaa zote hizo zitakuwa zikisafirishwa kuuzwa nje ya nchi  ambako kuna soko kubwa, wakati mkojo na mavi ya wanyama hao yatauzwa nchini kwa matumizi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mutua, kampuni yake inakusudia kusafirisha tani mbili za nyama ya sungura kila siku kwenda kuuzwa nje ya nchi, hivyo kufanya kiasi kwa mwaka mmoja kufikia tani 720.

Alisema mbali na sungura, kampuni yake inakusudia kuanzisha hoteli mahsusi kwa ajili ya uuzaji wa bidhaa zinazotokana na sungura pekee.

Utekelezaji wa mradi wa sungura kupitia Namaingo, utahusisha mafunzo ya kitaalamu kwa wafugaji yatakayotolewa kwa ushirikiano na watalaamu kutoka Suma JKT na Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA).

Akizungumza katika uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Donald Bombo alisema hatua iliyofikiwa na Mkurugenzi wa Namaingo, Ubwa Ibrahim kuanzisha mradi huo ni ya ujasiri na uthubutu unaolenga  kuwanufaisha wananchi na kuinua vipato vyao.

Bombo aliahidi kuwa, serikali itakuwa bega kwa bega kuhakikisha mipango ya kusaidia kiuchumi wananchi inafanikiwa.

Alisema ujenzi wa machinjio ya kisasa ya sungura unadhihirisha umoja na ushirikiano thabiti wa wafanyabiashara katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika uzinduzi huo, jumla ya sungura 600 waligawiwa kwa vikundi 20  vya wajasiriamali wa Mkoa wa Dar es Salaam.


No comments: