Mashindano ya kombe la Standard Chartered yaliyokuwa yanafanyika nchini Uingereza yamemalizika na kombe hilo kutwaliwa na timu ya nchini Singapore.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa kuwasili timu ya Azania iliyowakilsiha nchi za Afrika ya Mashariki, Meneja Uhusiano wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Mariam Sezinga amesema timu ya Azania ilikwenda Uingereza kushindana kwenye mashindano ya “Standard Chartered-Road to Anfield” iliyokuwa inahusisha wateja wa benki hiyo. Timu zilizoshiriki kwenye mashindano hayo zilikuwa ni timu nane kutoka Singapore, Uingereza, India, Nigeria, Botswana, Honk Kong, Korea na Tanzania.
Meneja Uhusiano wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Mariam Sezinga (nguo nyeusi) akiwasili na Wachezaji wa Timu ya Azania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam wakitokea nchini Uingereza kwenye mashindano ya kombe la Standard Chartered-Road to Anfield 2017.
Katika michuano hiyo timu ya Azania iliweza kutinga nusu fainali ambapo ilicheza na Uingereza na kutolewa kwa mikwaju ya penati. Timu ya Singapore iliibuka mabingwa wa kombe Standard Chartered –Road to Anfield kwa mwaka 2017. Mariam alisema timu hiyo imefanya vizuri kwenye mashindano hayo japo hawakufanikiwa kutwaa kombe hilo mara baada ya kutolewa kwenye michuano hiyo. Alisisitiza wao kama Benki ya Standard Chartered Tanzania hawajakata tamaa na hii ilikuwa ni fursa nzuri kwa vijana kuonesha vipaji vyao ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Na pia ameipongeza timu ya Azania kuiwakilisha vyema Tanzania kwa kuwa ni mara ya kwanza kuingia kwenye mashindano hayo na pia wamejitahidi kupigana mpaka kufikia kuingia nusu fainali ya mashindano hayo. Nahodha wa timu ya Azania, Khalid Sultan Said ameishukuru benki ya Standard Chartered Tanzania kwa kuona umuhimu wa michezo hapa nchini na wameweza kujifunza mengi kwenye michuano hiyo iliyokuwa ikiendeshwa nchini Uingereza ambapo timu yao ilitolewa kwenye nusu fainali. Lakini wao wanaamini hapa ni mwanzo na watapigana mpaka siku kombe liweze kutua hapa nchini.
Wachezaji wa timu ya Azania wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakitokea nchini Uingereza.
Meneja Uhusiano wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Mariam Sezinga (wa tatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wachezaji wa Timu ya Azania mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam wakitokea nchini Uingereza kwenye mashindano ya kombe la Standard Chartered-Road to Anfield 2017.
Wachezaji wa Timu ya Azania wakiwasiliana na ndugu jamaa na marafiki mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakitokea nchini Uingereza.
No comments:
Post a Comment