Moja ya ndege aina ya Helkopta ilipowasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya utoaji wa Huduma ya Utafutaji na uokoaji kwa wapanda Milima
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kilimanjaro SAR ya mkoani Kilimanjaro Ivan Broun akionekana mwenye tabasamu mara baada ya moja ya ndege aina ya Helkopta kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya utoaji wa Huduma ya Utafutaji na uokoaji kwa wapanda Milima.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini .
KAMPUNI ya Kilimanjaro SAR ya mkoani
Kilimanjaro imeanza rasmi shughuli za utafutaji na uokoaji kwa wapandaji wa
Milima miwili ya Kilimanjaro na Meru kwa kutumia ndege aina ya Helkopta.
Kilimanjaro SAR inakua kampuni ya kwanza kuweka
historia katika bara la Afrika ya utoaji wa huduma hiyo muhimu na maada kwa maisha ya wapandaji
wa Milima ikizingatiwa asilimia 75 ya magonjwa uwapo mlimani yanatokana na
mbadiliko ya Hali ya Hewa kulingana na urefu wa Mlima.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Afisa
mtendaji mkuu wa Kampuni ya Kilimanjaro SAR,Ivan Braun raia wa Denmark ameeleza
kuwa kuanza kwa shughuli hiyo kutasaidia
aliyepata matatizo akiwa mlimani kuhudumiwa ndani ya dakika 5 baada ya kupokea
simu ya hitaji la msaada.
“Kampuni hii itatoa huduma kamili ya uokoaji
wa dharura kwa wapanda Mlima,Takwimu zinaonyesha zaidi ya watalii 45,000
hutamani kupanda kilele cha mlima mrefu Africa, kwa bahati mbaya hofu juu ya usalama
wa maisha yao imekua kizuizi kwao kutimiza ndoto hii.”imeeleza sehemu ya
taarifa hiyo.
“Mabadiliko chanya sasa yamepatikana kutoka
katika huduma za uokoaji zisizo na ufanisi mpaka zenye ubora wa hali ya juu.”alieleza
Braun ambaye ni mtaalamu wa kupanda Milima.
Alisema mbali na kuwa na
Helikopta bora na zenye uwezo wa juu maalumu kwa huduma hiyo ya utafutaji na uokoaji pia ina timu maalumu ya
madaktari wa kimataifa na wasaidizi wa kliniki.
“Kampuni hii inaleta usalama
katika maana pana zaidi kwa kuanzisha kliniki ya kwanza Afrika maalumu kwa matibabu
ya magonjwa yatokanayo na mlima.Kampuni ya Kilimanjaro SAR itahakikisha inaifanya
Kilimanjaro kuwa sehemu salama zaidi ya utalii Africa.”alisema Braun.
Kuanza kwa utolewaji wa
huduma hiyo kutasaidia sekta ya Utalii nchini kupata suluhu ya
Changamoto ya muda mrefu ya utoaji wa msaada wa kitabibu, utafutaji na uokoaji
wa wageni wanaopata matatizo wakati wa kupanda Mlima Kilimanjaro na Meru .
Hivi karibuni kampuni ya
Kilimanjaro SAR iliingia makubaliano na Hospitali ya St Joseph ya mjini Moshi kuanza
kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa watakao pata matatizo wakati wa kupanda
Milima hiyo zoezi lililoenda sambamba na uzinduzi wa Kliniki ya kwanza Afrika
ya magonjwa yatokanayo na muinuko wa juu.
Katika uzinduzi huo mgeni rasmi ,Mkuu wa wilaya ya
Moshi ,Kippi Warioba alisema hii ni fursa mpya kwa sekta ya Utalii kuutangaza
vyema Mlima Kilimanjaro kwamba kwa kiasi
kikubwa itasaidia katika kuongeza idadi ya Watalii.
Hata hivyo kuanza kwa huduma hiyo muhimu kwa sekta ya
Utalii nchini ,bado ipo changamoto ya matumizi ya uwanja mdogo wa ndege wa
Moshi hali inayowalazimu kutumia uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro
(KIA).
No comments:
Post a Comment