‘GSMA Mobile Money Certification’ inatoa muongozo ili kuhamasisha utoaji wa huduma bora zaidi za kifedha kwa wateja wetu.
Dar es Salaam, 13 Aprili, 2018.
Tigo Pesa, huduma ya kifedha kwa simu za mkononi inayoongoza nchini, imepokea uthibitisho wa kimataifa ujulikanao kama ‘GSMA Mobile Money Certification’.
Uthibitisho huu unatambua uwezo mkubwa wa Tigo Pesa katika kutoa huduma salama, kwa uwazi, za kuaminika na thabiti zinazokuza haki za wateja na kuzuia miamala ya kihalifu.
Tigo Pesa ni moja kati ya watoa huduma za kifedha kwa simu za mkononi wa kwanza kabisa duniani kupokea uthibitisho huu kutoka GSMA.
GSMA Mobile Money Certification’ ni mkakati wa kimataifa unaolenga kuleta huduma za kifedha salama, wazi na thabiti zaidi kwa mamilioni ya watumiaji wa huduma za kifedha kwa simu za mkononi duniani kote. Huku kukiwa na zaidi ya akaunti 690 milioni za fedha kwa simu za mkononi duniani, sekta ya simu za mkononi inaboresha maisha duniani na imewezesha mamilioni ya watu wasiokuwa na akaunti za benki kufikiwa na huduma rasmi za kifedha.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Afisa Mkuu wa Huduma za Kifedha kwa Simu za Mkononi wa Tigo, Hussein Sayed alisema, “Tigo Pesa inajivunia mchango wake mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha nchini kwa kutoa fursa kwa mamilioni ya Watanzania wasio na huduma za kibenki kuwa sehemu ya mfumo rasmi wa kifedha.’
Uthibitisho huu kutoka GSMA ni ishara tosha kuwa Tigo Pesa imepiga hatua kubwa kuhakikisha kuwa fedha za wateja wetu zipo salama, na kuwa haki zao zinalindwa. Kupitia taratibu zetu za kibiashara tunalenga kutoa huduma zenye viwango vya juu zaidi.
GSMA imebainisha kuwa vigezo vinavyotumika kutoa uthibitisho huu vinazingatia viwango vya ubora wa kimataifa katika utoaji huduma za kifedha. Kabla ya kupokea uthibitisho huo, kila mtoa huduma wa fedha kwa njia ya simu za mkononi sharti afikie asilimia 100% ya vigezo vilivyowekwa. Watoa huduma wanaopokea uthibitisho huu ni wale tu waliofanikiwa kuonesha kuwa hatua za uendeshaji wa biashara zao ni miongoni mwa zile zilizo bora, zinazoaminika na kuwajibika zaidi katika mfumo mzima wa utoaji huduma za kifedha duniani.
“Tigo Pesa inajivunia kufikia vigezo vilivyotuwezesha kupokea uthibitisho huu kutoka GSMA. Hii inaonesha ubora na uwajibikaji katika huduma zetu. Vile vile inathibitisha kuwa tunaongoza katika mageuzi ya kidigitali na utoaji wa huduma za kifedha ulimwenguni,’ Hussein aliongeza.
Pamoja na azma ya Tigo kutoa huduma za kiwango cha kimatifa kwa wateja wetu, huduma yetu ya Tigo pesa imeboreshwa na kuwa mfumo kamili wa huduma za kifedha. Daima tupo mstari wa mbele katika ubunifu wa huduma katika soko hili; kwa mfano tulikuwa mtoa huduma wa kwanza duniani kuzindua huduma ya fedha kwa simu za mkononi iliyowezesha uhamishaji wa fedha kwenda mitandao mingine nchini. Pia tulianzisha huduma ya kwanza Afrika Mashariki iliyowezesha wateja kufanya miamala ya fedha kupitia simu za mkononi kwenda nje ya nchi kwa kubadili thamani ya fedha kwa sarafu ya nchi husika. Tigo pia ndio kampuni ya kwanza ya simu za mkononi kutoa gawio la faida kwa wateja wetu.
‘Uthibitisho huu wa GSMA unaashiria uendeshaji wa biashara yetu unazingatia mojawapo ya mifumo bora zaidi duniani. Tigo Pesa inaaminika na kuwajibika, hivyo ni mshirika bora wa kibiashara,’ Afisa huyo Mkuu wa Huduma za Kifedha kwa Simu za Mkononi wa Tigo alibainisha.
‘GSMA Mobile Money Certification’ unaonesha mwamko mkubwa kwa upande wa watoa huduma kuzuia utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi; pamoja na kutoa huduma bora, za uhakika, salama na zisizokuwa na upendeleo kwa wateja na washirika wote wa kibiashara.
No comments:
Post a Comment