Tangazo

August 25, 2011

Waasi Libya watangaza donge nono la Dolla Milioni 1.7 kwa atakayemkamata au kumuua Gaddafi

Kiongozi wa Libya, Col. Muammar Gaddafi
Waasi nchini Libya wametangaza kutoa msamaha kwa mtu yeyote atakayemkamata au kumuua Kanali Muammar Gaddafi na kutangaza zawadi ya dolla million 1.7.

Kiongozi wa Baraza la Kitaifa la Mpito (NTC), Mustafa Abdel Jalil, alielekeza msamaha huo kwa wandani wa Kanali Gaddafi. Alitoa tangazo hilo akiwa mjini Benghazi, mashariki mwa Libya.

''Wanajeshi wa Kanali Muammar Gaddafi na wanaomuunga mkono hawatasitisha mapigano hadi pale Gaddafi atakapo kamatwa au kuuwawa'', Bw Abdel Jalil alisema.

Naye msemaji wa waasi ameiambia BBC kuwa mazungumzo yanaendelea kati yao na viongozi wa makabila katika maeneo mbali mbali kutafuta suluhu la mzozo huo.

Aidha, uongozi wa waasi umeahidi kukubali Kanali Gaddafi aondoke salama nchini humo ikiwa ataachia madaraka.

Bado haijulikani alipo Kanali Gaddafi, japo waasi wamesema wanadhani bado yuko mjini Tripoli.

Makabiliano makali yameendelea mjini Tripoli kati ya waasi na wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi.

Kiongozi huyo wa Libya ambaye hajulikani aliko aliapa kupitia hotuba iliyopeperushwa kupitia redio moja ya kitaifa kuwa, yuko tayari kupigana hadi ashinde au afe.

Jumanne, waasi walishika udhibiti wa makazi yake ya Bab al-Aziziya.

Wanajeshi wa Kanali Gaddafi bado wanadhibiti mji wa Sirte, alikozaliwa kiongozi huyo wa Libya.
Afrika Kusini bado haitambui waasi.

Wakati huo huo, Mgororo wa kidiplomasia umeibuka katika kikao cha Umoja wa Mataifa na kukwamisha juhudi za Marekani za kupata idhini ya kuwapa waasi hao dola billioni moja na nusu, amana ya serikali ya Libya.

Hii ni baada ya Afrika Kusini, ambayo ilijaribu kuwa mpatanisha katika mzozo huo, kusema kuwa bado inangonja muongozo kutoka kwa Muungano wa Afrika , ambao bado haujatambua uongozi wa waasi kama wawakilishi halisi wa watu wa Libya.

Balozi wa Afrika Kusini katika umoja wa mataifa, Baso Sangqu, amesema wana wasiwasi kuwa kulifadhili baraza hilo la waasi kutamanisha kuitambua rasmi kama serikali ya nchi hiyo.

''Bado hatujachukua uamuzi kufikia sasa kuhusu kutambua waasi kama wawakilishi pekee wa watu wa Libya na azimio hilo la Umoja wa Mataifa linasema kuwa pesa hizo lazima ziende kwa watu wa Libya'', Balozi Baso Sangqu alisema.

Marekani inasema pesa hizo zinahitajika kwa dharura ili kutoa misaada ya kibinadamu.

Baraza la Mpito la Kitaifa nchini Libya linakadiria kuwa takriban watu 400 wameuwawa na maelfu kujeruhiwa katika mapigano ya kudhibiti mji wa Tripoli, tangu siku ya Jumapili.BBC Swahili

1 comment:

Anonymous said...

Huyu jamaa si wa kumuua ni wa kumkausha halafu anawekwa katika maonyesho Libya watatajirika zaidi kwa kupata watalii toka pande zote za dunia kumuona huyu jamaa, Au awekwe awe mchekeshaji aktika mikutano ya taifa na tv.