Tangazo

September 7, 2011

Mwanasoka Nizar Khalfan aishukuru Serikali ya Rais Kikwete

Mtanzania anayecheza Soka ya kulipwa katika timu ya White Caps ya jijini Vancouver Canada, Nizar Khalfan akimkabidhi Rais Dk. Jakaya Kikwete jezi ya timu yake wakati alipokwenda kumsalimu na kumshukuru Ikulu jijini Dar es Salaam juzi jioni. PICHA/IKULU  
                                            
                                     *********************************

Mchezaji maarufu wa soka wa kimataifa wa Tanzania, Nizar khalfan,  ameishukuru Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa misaada mingi ambayo Serikali hiyo imekuwa inatoa kwa wanamichezo, wakiwemo wanasoka na hatua
nyingine za Serikali hiyo kuunga mkono jitihada za wanamichezo wa Tanzania.

Aidha, Nizar Khalfan amemshukuru Rais Kikwete kwa jitihada binafsi ambazo hatimaye zimechangia katika mafanikio ya Nizar Khalfan katika soka. Mwanasoka huyo wa Tanzania sasa anacheza soka ya kulipwa katika timu ya Whitecaps ya Canada.

Mwanamichezo huyo alimmwagia sifa Rais Kikwete na Serikali yake wakati alipokutana na kufanya naye mazungumzo ya ana kwa ana juzi jioni Ikulu, Dar es salaam.

Mwanamichezo huyo pia alimkabidhi Mheshimiwa Rais Kikwete jezi ya timu ya Whitecaps – Jezi Nambari Nne (04) – ikiashiria kuwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ni Rais wanne wa Tanzania.

Katika mkutano wake na Mheshimiwa Rais, mwanasoka huyo aliandamana na wafadhili wengine wa soka akiwamo Bwana Rahim Kangezi na Bwana Robert Slavik ambaye pia ni Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za uchimbaji madini ya Ruby Creek Resources yenye shughuli zake katika wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi.

Katika mazungumzo hayo, Nizar Khalfan, mbali na kumshukuru Rais Kikwete na Serikali yake, pia amemwelezea kiongozi huyo kuhusu maendeleo yake ya soka katika medani ya soka ya kulipwa nchini Canada na matumaini yake ya baadaye.

“Mheshimiwa Rais, sasa Mungu ananisaidia kwa sababu napata nafasi zaidi ya kucheza katika timu yangu,” Nizar Khalfan alimwambia Mheshimiwa Rais na kuongeza kuwa shabaha na nia yake hasa ni kupata nafasi ya kucheza katika ligi kubwa na ngumu zaidi za Ulaya.”

Mheshimiwa Rais alimshukuru Nizar Khalfan kwa kuiwakilisha vizuri Tanzania nchini Canada akisisitiza: “Nakutakia kila la heri. Mnatuwakilisha vizuri na tunapata heshima kubwa kwa sababu yenu. Jitahidini zaidi kwa sababu
mnailetea Tanzania heshima kwa mafanikio yetu. Tunafurahia mafanikio hayo na tunakushukuru kwa kuja kututembelea.”

Nizar Khalfan yuko nchini tokea wiki iliyopita ambako alikuja kuiwakilisha Tanzania katika michezo ya awali ya Kombe la Soka la Mataifa ya Afrika dhidi ya Algeria. Timu hizo mbili zilitoka sare 1-1 katika mechi hiyo kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nizar Khalfan amekuwa anaichezea klabu ya Whitecaps iliyoko katika Ligi Kuu ya Marekani na Canada ya MLS kwa miaka mitatu sasa. Kabla ya kuondoka nchini alipata kuchezea timu za Mtibwa Sugar na Moro United.

Julai 17, mwaka huu, 2011, alikuwa katika kikosi cha Whitecaps kilichopambana na timu ya klabu ya England ya Manchester City ambako Whitecaps walilala kwa bao 1-0.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM

No comments: