Tangazo

September 26, 2011

" Wanafunzi msichanganye Elimu na Mapenzi" asema Mama Salma Kikwete

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo

Wanafunzi nchini wametakiwa kuachana na tabia ya kujiingiza katika mapenzi wakiwa  masomoni kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanahatarisha maisha yao kwa kupata maambukizi ya Virusi vinavyosababisha Ugonjwa wa Ukimwi na ujauzito.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Barbro Johansson iliyopo Luguruni jijini Dar es Salaam kwenye  sherehe za mahafali ya kidato cha nne na  cha sita.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwaambia wanafunzi hao  kuwa elimu wanayoipata  itafungua maisha yao na ya jamii nzima. Itawapa njia ya kuwa na uwezo kiuchumi, itawajengea uwezo wa kujiamini na  kuweza kupaza sauti zao na kusikika kwani watakuwa na upeo mkubwa wa kuchambua mambo na kutoa maamuzi ya busara katika maisha.

 “Ninafahamu kwamba walimu, wazazi na walezi wamekuwa wakiwausia na kuwapa miongozo katika maisha yenu ya kutafuta elimu. Jambo ambalo ningependa muendelee kulizingatia kwa makini ni kwamba elimu mliyoipata bado ni mwanzo tu, hasa ukizingatia kukua kwa utandawazi.

Siku hizi mabadiliko ni ya haraka mno na yanamgusa kila mtu katika kila nyanja ya maisha. Ni vizuri mkajua kwamba ni wajibu wenu kuendelea kujifunza mbinu mpya za kuyakabili mabadiliko haya”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alimalizia kwa kuwataka wanafunzi hao kuchukua tahadhari dhidi  ya ugonjwa wa Ukimwi kwani elimu waliyonayo  haitakuwa na maana kama wataruhusu kuambukizwa ugonjwa huo na kupata ujauzito ambao utawafanya wakatize masomo yao na hivyo kutotimiza ndoto zao.

Akisoma taarifa ya shule hiyo  Mkuu wa Shule  Halima Kamote alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa shule hiyo miaka 11 iliyopita  jumla ya wahitimu 471 wa kidato cha nne na 282 wa kidato cha sita walihitimu masomo yao na kufaulu kwa kiwango cha juu na kufanikiwa kujiunga na vyuo mbalimbali na vya elimu ya juu hapa nchini.

Kamote alisema , “Katika mahafali ya leo tunao wahitimu 76 wa kidato cha nne na 151 wa kidato cha sita ambao tunaamini  kutokana na elimu  waliyoipata kutoka kwa walimu wao watafanya vizuri katika mitihani yao ya kitaifa na hivyo kuendelea kutunza heshima ya shule yetu katika jamii”.

Shule hiyo yenye  wanafunzi 632 wa kidato cha kwanza hadi cha sita, walimu 37 na wafanyakazi wengine 27 imekuwa ikipata msaada kutoka Serikali ya Sweden kupitia ubalozi wake hapa nchini ambao umetumika  kujenga majengo, matanki ya kuhifadhi maji na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wenye vipaji kilaaluma ambao wanatoka katika familia  zenye kipato duni.

Alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa majengo, wafadhili wakuu wa shule hiyo ambao ni SIDA wanatarajia kukatisha ufadhili wao mwishoni mwa mwaka huu na hivyo kuzua tatizo la kukosekana kwa ufadhili wa uhakika wa ada kwa wanafunzi wanaotoka katika familia duni.

“Changamoto nyingine zinazotukabili ni wanafunzi wanaofadhiliwa na shule hii wanakosa mikopo pale wanapojiunga na elimu ya juu pengine ni kwa kuwa wanatoka katika shule binafsi ambako kuna ulipaji wa ada unaoendana na gharama halisi na  mahitaji ya kujiunga na shule ni makubwa kuliko uwezo wa shule”, alisema.

Kila mwaka sherehe za mahafali ya shule hiyo hufanyika tarehe 25 Septemba ili kuienzi siku aliyozaliwa Dk. Mama Barbro Johansson ambaye ni mmisionari, mwalimu, mwanaharakati na mwanadiplomasia kutoka nchini Sweden ambaye alitoa mchango mkubwa katika kupigania elimu ya watoto wa kike na wa kiume.

No comments: