Rais Jakaya Mrisho Kikwete |
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani salamu za rambirambi na masikitiko makubwa kufuatia ajali ya basi la abiria lijulikanalo kama Delux Coach iliyotokea jana tarehe 25.10.2011.
“Hii ni ajali mbaya sana, ni ajali ya kusikitisha sana na ya kuhuzunisha kwa wananchi wote na hasa mimi” Rais amesema na kusisitiza kuwa ajali kama hizi zinazidi kutoa changamoto kwa Polisi na Vyombo vya Usalama Barabarani.
“Huu ni mtihani zaidi kwa Polisi na Vyombo Vya Usalama Barabarani, tunahimiza sheria za barabarani zifuatwe na kuzingatiwa, na hili ni pamoja na usalama wa vyombo hivyo na abiria wake, hii ni changamoto kubwa kwa polisi katika kulisimamia hili na kuona linatekelezwa” Amesema.
Rais amezidi kuwakumbusha Polisi wa Usalama Barabarani kutolegeza kamba au kuwa waangalifu tu pale ajali inapotokea na kulegeza kamba mara baada ya tukio kuisha.
“Hili ni eneo ambalo litazidi kuwa tatizo siku hadi siku kama hamtakuwa makini na kuonesha ushupavu kwa wale wote wanaovunja sheria na kutozingatia mahitaji ya chombo salama cha usafiri wa binadamu na mali zao wakati wote”. Amesisitiza.
“Nawapa pole wafiwa wote, nawatakia waliojeruhiwa kupata ahueni haraka iwezekanavyo na kurudi katika shughuli zao za kila siku.” Rais amesema.
Kulingana na taarifa ya awali ya Polisi, Basi lilipasuka tairi la mbele kulia, likaachia njia na kusababisha kupinduka na ghafla likawaka moto na kusababisha vifo na majeruhi.
Ajali hiyo imetokea katika eneo kati ya Kongowe na Misugusugu kwenye barabara kuu ya Dar-Morogoro ambapo basi hilo lilitokea Dar kuelekea Dodoma.
Taarifa inasema basi liliondoka Dar likiwa na abiria 42 na kufika Kibaha lilipakia wengine watano, hivyo pamoja na dereva na utingo basi likawa na abiria 49 wakati wa ajali.
Hadi sasa taarifa kamili ya waliopoteza maisha bado haijathibitishwa kutokana na basi kuungua na kusababisha kuungua kwa baadhi ya abiria, ambapo mafuvu matano yameokotwa katika eneo la ajali na watu 8 hawafahamiki waliko.
Taarifa inaendelea kueleza kuwa abiria 36 inasemekana wamejiokoa kwa kupitia madirishani baada ya kupata maumivu, kati yao wanaume 27 na wanawake 9 wote wamepelekwa katika hospitali teule ya Tumbi ambapo wanawake wawili wamelazwa na wengine wametibiwa na kuruhusiwa.
IMETOLEWA na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu.
Dar es Salaam.
26 Oktoba, 2011
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu.
Dar es Salaam.
26 Oktoba, 2011
No comments:
Post a Comment