Tangazo

October 18, 2011

T-MOTO KUANZA NA MOTO BAADA YA UZINDUZI WA KUNDI NA ALBAM YA KWANZA

*Kutoa msaada wa kitanda cha kuzalia wajawazito katika Hospitali ya Mkoa Mtwara

KUNDI jipya la taarab linalokuja kwa kasi nchini, Tanzania Modern Taarab (T-Moto) ama ‘Real Madrid’ linatarajia kuanza kufanya maonyesho mawili katika mkoa wa mtwara.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi wa kundi hilo, Amini Salmini, alisema kuwa  mara tu baada ya uzinduzi wa kundi hilo unaotarajia kufanyika Oktoba 28, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, kundi hilo tayari linamwaliko wa Oktoba 29 na 30, Mkoani Mtwara.

Aidha alisema kuwa mara tu baada ya kumaliza onyesho la uzinduzi huo, wasanii wataondoka jijini usiku huo huo kuanza safari ya kuelekea Mtwara ambako watafanya maonyesho mawili.

Onyesho la kwanza la oktoba 29, linatarajia kufanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Makonde Beach Club, na onyesho la pili litafanyika Oktoba 30 Nachingwea.

Pia Salmini alisema kuwa kabla ya kufanya onyesho la pili wasanii wa kundi hilo watatembelea wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa huo husasan wodi ya wazazi na watoto, ambapo watatoa msaada wa kitanda cha kuzalia cha wajawazito katika hospitali hiyo pamoja na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto waliolazwa katika hospitali hiyo.

Aidha katika uzinduzi wa kundi hilo unaotarajia kufanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Bendi za Mapacha Watatu na Msondo Ngoma, zitakuwa bega kwa bega katika kutoa burudani za kusindikiza na ‘kusapoti’ kundi hilo.

“Tayari maandalizi yote ya uzinduzi yamekamilika ikiwa ni pamoja na mazoezi ya kutosha wanayoendelea nayo wasanii wa kundi letu ambao hadi sasa wapo Kambini wakitarajia kuvunja kambi siku moja kabla ya uzinduzi” alisema Amini.

Albam hiyo ya kwanza ya kundi hilo imebebwa na wimbo wa Bi Mwanahawa Ally, uitwao Aliyeniumba Hajanikosea, ambapo pia itakuwa na nyimbo nyingine kali zilizoanza kusikika katika vituo mbalimbali vya redio.

Nyimbo nyingine ni wimbo wa Jokha Kassim, ambao tayari umeshaanza kuzua gumzo miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Taarab, ambao hauishi kujadiliwa, uitwao Unavyojidhani Hufanani.

 Nyingine zinazokamilisha albam hiyo ni pamoja na Mchimba Kaburi Sasa Zamu yake Imefkuwa ni ‘Dongika, ulioimbwa na Mrisho Rajab, aliyejitosa katika fani ya muziki wa Taarab akitokea katika shindano la BSS, pamoja na Riziki Shotcut, ulioimbwa na Aisha Masanja.

No comments: