Tangazo

October 20, 2011

Watanzania watakiwa kujenga moyo wa kujitolea kufanya kazi

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo

 Watanzania wametakiwa kujenga tabia ya kujitolea kufanya kazi kwa moyo na kushiriki katika shughuli za kujiongezea kipato  kwa lengo la kujikwamua kimaisha  kwani hakuna mafanikio yatakayopatikana bila ya kujitolea na kufanya kazi kwa bidii.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizindua Umoja wa Vikundi vya kuweka Akiba na Kukopa vilivyopo chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) katika kata ya Majohe wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema kuwa kabla ya kupatikana kwa Uhuru wa Tangayika kuna watu ambao walijitolea bila ya kulipwa chochote kupigania Uhuru  na nchi ikawa huru hivyohivyo kwa viongozi wa vikundi hivyo wamekuwa wakijitolea kufanya kazi ndiyo maana vikundi vimefika hapo vilipo hivyo basi ni muhimu kwa wanachama wa umoja huo kutenga muda wao kwa kufanya kazi za maendeleo.

“Ninawaasa  ili muweze kuendeleza umoja wenu ni lazima muwe  na ushirikiano na upendo  miongoni mwenu,  muwe waaminifu katika suala la utunzaji wa fedha na siri  kwani kukosa uaminifu ni jambo litakalosababisha migongano baina yenu kwani katika sehemu mbalimbali vikundi vingi vya kijamii huvunjika baada ya muda fulani kutokana na kukosa shughuli za kudumu, muundo usiokuwa mzuri na usimamizi ambao si madhubuti” alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kusema kuwa Taasisi yake  inatambua umuhimu wa kumuwezesha mwanamke kwa njia ya kumjengea uwezo, kumpa mafunzo na kumuunganisha na watoa huduma  ndiyo maana vikundi hivyo vilianzishwa ili kuwawezesha wanawake pamoja na wanaume wanaopenda kushiriki kuweza kupata huduma za kimaendeleo na kujengewa uwezo katika nyanja mbalimbali.

Akisoma taarifa ya umoja huo Juliana Remmy ambaye ni Mwenyekiti alisema kuwa  walikuwa wakiendesha vikundi vyao kila kimoja na utawala wake na kujitegemea lakini chini ya Taasisi ya WAMA wameungana  kwa pamoja na kupata muundo ambao unajumuisha vikundi vyote na hivyo imekuwa rahisi kujadiliana, kushirikiana na kuwasiliana kwa urahisi.

Remmy alisema kuwa malengo waliyonayo ni kuwa na mfuko wa pamoja ambao utawawezesha kutatua matatizo ya kijamii ambayo vikundi vidogo havitaweza kuyatatua, kuongeza mtaji ili kuweza kuanzisha SACCOS ambayo itaweza kuwasaidia kukopeshana mikopo mikubwa na ya muda mrefu na kujenga jengo la ofisi.

“Changamoto zinazotukabili ni elimu ndogo ya uongozi na ujasiriamali, upungufu wa masanduku ya kutunzia fedha kwa ajili ya vikundi vipya vinavyoanzishwa, ukosefu wa vifaa vya ofisi   na upungufu wa fedha za kuendesha umoja wetu”, alisema Mwenyekiti wa umoja huo.

Aliyataja mafanikio waliyoyapata kuwa ni kuweka akiba na kupeana mikopo midogo midogo ambayo huwaingizia faida wanayogawana mwisho wa mwaka, wameweza kujifunza kusindika  siagi ya karanga, achali ya embe na mbilimbi, kutengeneza mifuko ya karatasi na kuunganishwa na wajasiriamali wa kati ambao wamewaelimisha namna ya kutengeneza bidhaa bora zenye kukidhi mahitaji ya soko.

Mwaka 2009 Mama Tabu Likoko ambaye ni Afisa Uwezeshaji kitengo cha Wanawake kutoka WAMA alianzisha kikundi kimoja katika kata hiyo hadi kufikia mwaka huu kumekuwa na vikundi 40 vyenye wanachama 700 katika kata ya Majohe  na maeneo ya mwisho wa lami, Magomeni, Gongo la Mboto, Vituka, Tabata na Temeke.

Zaidi ya shilingi milioni nane, kompyuta , ahadi za mabati na upatikanaji wa kiwanja cha kujengea ofisi zilitolewa  na  wadau mbalimbali wa maendeleo waliohuduria katika sherehe hizo.

No comments: