Tangazo

November 3, 2011

NG'OMBE AZAA NDAMA MWENYE MIGUU MITATU -SINGIDA

Mzee Yuda Memba mkazi wa Kitongoji cha Ikusi "B", Kata ya Mwankoko katika Manispaa ya Singida akiwa na ndama wake aliyezaliwa akiwa na miguu mitatu na ambaye amefikisha umri wa wiki tatu sasa.

Ndama aliyezaliwa na miguu mitatu.

Mzee Yuda akiwa na ndama wake pamoja  na familia yake. Na picha nyingine ya pamoja ni familia ya mzee Yuda. PICHA ZOTE/JUMBE ISMAILLY- SINGIDA

                                     ************************************************

 Na Jumbe Ismailly, Singida

WAFUGAJI wa mifugo mbalimbali katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida wametakiwa kuondokana na imani za kishirikina,mifugo yao inapozaa viumbe ambavyo havina baadhi ya viungo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikusi “B”,kata ya Mwankoko,katika Manispaa ya Singida,Bwana Jumanne Mdigida alitoa wito huo  kufuatia tukio la ng’ombe wa mfugaji mmoja wa kitongoji hicho kuzaa ndama mwenye miguu mitatu badala ya minne.

Alifafanua mwenyekiti huyo kwamba uzoefu unaonyesha kwamba baadhi ya wafugaji kwenye maeneo ya Kijiji na kata hiyo wamekuwa na utamaduni wa kutoamini kwamba mnyama yeyote anaweza kuzaliwa akiwa na viungo pungufu kama vinavyotakiwa.

Akitoa mfano Bwana Mdigida alibainisha kuwa iwapo binadamu anaweza kuzaliwa akiwa na ulemavu,hivyo basi ni ukweli usiopingika kwamba hata wanyama pia wanaweza kuzaliwa wakiwa na upungufu huo wa viungo.

“Sasa iwapo kama binadamu wenyewe huzaliwa wakiwa na ulemavu wa baadhi ya viungo,hivyo hakuna shaka yeyote hata kwa wanyama nao kuzaliwa wakiwa na upungufu wa viungo vya sehemu Fulani ya mwili wake”alifafanua Bwana Kidigida.

Hivyo kutokana na tukio hilo ambalo ni la kwanza la aina yake kwa mfugaji wa mifugo hiyo,mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafugaji wa mifugo wenye imani za kishirikina na hata kufikia hatua ya kufikia maamuzi ya kuua,kuacha mara moja tabia na badala yake waendelee kuwatunza na kuhakikisha wanawapatia haki zao zote za msingi ikiwemo ile ya kusihi.

Kwa upande wao wafugaji ambao ng’ombe wao ndiye aliyezaa ndama mwenye miguu mitatu,Bwana Bonifasi Mwiko na Bwana Yuda Memba waliweka wazi kuwa baada ya ng’ombe wao huyo kuzaa kiumbe wa aina hiyo walipatwa na mshangao baada ya kuona miguu mitatu badala ya mine.

Hata hivyo wafugaji hao walisema ndama huyo ambaye alizaliwa wiki tatu zilizopita hivi sasa,ana hali nzuri na kwamba hana tatizo lolote linalomsumbua.

Kwa mujibu wa wafugaji hao ng’ombe aliyemzaa ndama huyo,huo ni uzao wake wa nne na kwamba ndama wengie watatu wana viungo vyote kama kawaida.

Akielezea tukio hilo,kaimu afisa kilimo na maendeleo ya mifugo wa Manispaa ya Singida,Dk.Nevil Mlinga aliweka bayana kwamba kuzaliwa kwa wanyama wa aina hiyo ni matukio ya kawaida yanayoweza kutokea kwa mfugaji wa mifugo yeyote ile.

Aidha daktari huyo wa mifugo alifafanua pia kuwa chanzo cha matukio ya aina hiyo mimba kutokukuwa vizuri,uzazi wa wanyama hao kuzaliana wao kwa wao bila kubadilishwa pamoja na baadhi ya madawa wanayopewa  kuchangia kuvuruga mfumo mzima wa uzazi.

No comments: