Tangazo

January 13, 2012

RAIS JAKAYA KIKWETE AMLILIA 'MZEE KIPARA'

Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amekitumia salamu za rambirambi Kikundi cha Sanaa cha Kaole kuomboleza kifo cha msanii maarufu na mkongwe, Mzee Fundi Saidi, maarufu kwa jina la kisanii la Mzee Kipara.

Katika salamu zake alizozitoa jana kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Kikwete amesema kuwa amesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha Mzee Fundi Saidi ambaye amemweleza kuwa alichangia sana maendeleo ya Tanzania kupitia shughuli zake wa usanii wa uingizaji.

Mzee Fundi Saidi, maarufu kwa jina la Bwana Kipara alifariki dunia asubuhi ya jana, Jumatano, Januari 11, 2012 nyumbani kwake Kigogo, Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 89.
Mzee Kipara enzi za uhai wake.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa habari za kifo cha Mzee Fundi Saidi. Sote tutamkumbuka kwa mchango wake mkubwa ambao alioutoa katika maendeleo ya nchi yetukupitia shughuli zake za usanii wa miaka mingi wa uingizaji.”

Ameongeza Rais Kikwete katika salamu zake, “Nawatumieni nyie wasanii wa Kikundi cha Kaole salamu zangu za rambirambi za dhati ya moyo wangu.

Napenda kuwaambia kuwa kifo cha Mzee Fundi Saidi kimelinyang’anya taifa letu na nyie wenyewe kisima cha uzoefu wa miaka mingi katika shughuli za sanaa.  Kwa hakika, Mzee wetu huyo amechangia sana maendeleo ya taifa letu kupitia shughuli za usanii wa uingizaji na ameacha mfano bora wa kuigwa katika kutumikia nchi yetu kwa kutumia vipaji vyetu.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda pia kupitia kwenu kutuma salamu zangu za rambirambi kwa wana-familia, ndugu na jamaa wa Mzee Fundi Saidi. Wajulishe kuwa niko nao katika wakati huu wa majonzi na namwaomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira kwa sababu yote ni mapenzi yake. Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Fundi Saidi. Amen.

No comments: