Tangazo

February 1, 2012

CCM yatoa Tamko kuhusu Mgomo wa Madaktari na Posho za Wabunge

Nape Moses Nnauye
Kwa muda sasa nchi yetu imepitia kwenye tatizo kubwa la mgomo wa madaktari katika hospitali nyingi hasa za umma ambao kwa kiasi kikubwa mgomo huo umekuwa na madhara makubwa kwa watanzania masikini ambao ni wengi, kiasi cha kugharimu hata maisha yao.

Chama Cha Mapinduzi kinachukua nafasi hii kuwapa pole sana wale wote walioathiriwa kwa namna moja ama nyingine na mgomo huu. Na kwakweli tunasikitishwa sana na hali inayoendelea!

Chama Cha Mapinduzi kinawapongeza na kuwashukuru madakitari walioonyesha ubinadamu na uzalendo kwa kuamua kurudi kazini na ambao hawakugoma kabisa. Tunawashukuru na kuwapongeza kwani hakuna masilahi yanayovuka thamani ya uhai wa binadamu mwenzako!

Tunachukua fursa hii pia kuwashukuru sana na kuwapongeza askari wetu wa jeshi la wananchi wa Tanzania kwa uamuzi wao wa kizalendo wa kuamua kuitikia wito wa serikali kwenda kwenye baadhi ya hospitali kusadia kuwatibu watanzania wenzao. Moyo huu ni wa kizalendo na wa mfano. Tunajivunia uzalendo wa jeshi letu!

Tunachukua nafasi hii kuwaomba madaktari wanaoendelea na mgomo kurudi kazini huku wakiendelea na mazungumzo na serikali. Tunaamini madai yao yanawezekana kushughulikiwa ikiwa pande zote mbili zitaamua kukaa chini kwa dhati na kuzungumza.

Serikali kwa upande mmoja watafute kwa makini chanzo cha mgogoro huu na kutafuta majibu, na madakitari nao kwa upande wa pili, wawe tayari kukaa mezani na kuzungumza. Tunasisitiza thamani ya maisha ya binadamu ni kubwa kuliko masilahi na madai wanayoyaomba!

Serikali ni vizuri ikajenga utamaduni wa kushughulikia matatizo haya ambayo yanaathiri wananchi wengi kwa uharaka na udharura unaostahili badala ya kusubiri hali inapokuwa mbaya zaidi.

POSHO ZA WABUNGE
 
Kwa upande mwingine Chama Cha Mapinduzi kinapenda kurudia wito kilioutoa juu ya swala la posho za wabunge. CCM iliwaomba na kuwasihi wabunge na mamlaka zinazohusika na mchakato wa swala hili kuliangalia upya na kutumia busara, ikiwezekana kuachana nalo kwasasa.

CCM inaupongeza na kuunga mkono msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kama ulivyonukuliwa na taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, kuwa ni vizuri wabunge wakalitafakari upya swala hili kwa masilahi mapana ya wale waliowapa dhamana ya kuwawakilisha bungeni.

CCM inaendelea kuwasihi waheshimiwa wabunge walitafakari upya swala hili na busara itumike katika kuliamua huku wakifungua masikio kusikiliza sauti za Watanzania kwani huko bungeni  wana wawakilisha hawa Watanzania, ni vizuri kusikiliza hiki kilio chao! Si busara kupuuza kilio cha waliokupa dhamana ya kuwawakilisha.

Msimamo wa Rais Kikwete kama sehemu moja ya mamlaka inayohusika na mchakato huo ni uthibitisho wa usikivu wake kwa wananchi anaowaoongoza, yeye katimiza wajibu wake, tunawasihi waheshimiwa wabunge wetu nao walitafakari hili na kuona busara ya kuachana nalo kwasasa.

Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM
Itikadi na Uenezi

No comments: