Tangazo

February 7, 2012

Rais Kikwete awapiga jeki 'Machinga' jijini Mwanza

Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewachangia wachuuzi wadogo wadogo wa mitaani (Wamachinga) wa mjini Mwanza sh. milioni 10, ili kuongeza nguvu katika mfuko wa kukopeshana wa wachuuzi hao.
 
Rais Kikwete ametoa uamuzi wa kuchangia mfuko huo wa uwezeshaji wa Wamachinga hao baada ya kusikiliza maelezo ya shughuli zao na jitihada zao za kuanzisha mfuko wenye raslimali za kutosha za kuwawezesha wanachama wa kikundi cha Wamachinga cha Mwanza kukopeshana kwa nia ya kuongeza mitaji ya kufanyia shughuli zao.

Akizungumza na viongozi wa Wamachinga hao waliokwenda kumwona katika Ikulu Ndogo ya mjini Mwanza leo, Jumatatu, Februari 6, 2012, Rais Kikwete amesema kuwa ni matarajio yake kuwa fedha hizo zitatumika vizuri na kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

“Mkiwezesha kunithibitishia kuwa fedha hizo zimetumika vizuri na kwa madhumuni yaliyokusudiwa basi tutaangalia jinsi gani ya kusaidia zaidi katika siku zijazo,” Rais Kikwete amewaabia Wamachinga hao katika mkutano ambao ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Evarist Ndikilo.

Wakati huo huo, Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Mwanza usiku wa jana alikutana na kuzungumza na wawakilishi wa wazee wa Mkoa wa Mwanza.

Katika mazungumzo hayo, wazee hao chini ya Mwenyekiti wao wa muda, Mzee Charles Masakulangwa wamemweleza Rais Kikwete kuhusu mipango yao mbali mbali ukiwamo mradi wa ujenzi wa afya wa hospitali.

Mchana huu, Rais Kikwete amewasili mjini Dodoma kwa ziara nyingine ya kikazi baada ya kumaliza ziara ya Mwanza.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.


No comments: