Tangazo

February 10, 2012

MAAMUZI YALIYOFIKIWA NA MADAKTARI FEBRUARY 9, 2012 KUFUATIA MKUTANO KATI YAO NA WAZIRI MKUU MHE. MIZENGO PINDA KATIKA UKUMBI WA CPL, HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI.

Dr. Ulimboka Stephen
Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari nchini inapenda  kuwajulisha madaktari wote pamoja na kada nyingine zote za afya nchini  juu ya kile ambacho kimejiri katika siku  ya tarehe 09.02.2012  ikiwa ni matokeo ya kikao wanataaluma wa kada za afya na Waziri Mkuu  Mhe. Mizengo Pinda na baadaye kufuatiwa na kikao kati ya madaktari na  kada nyingine za afya.

Ifahamike kuwa kama Kamati tulipata mwaliko wa kushiriki katika  Mkutano huo ambapo ilitarajiwa kuwa Mhe, Waziri mkuu atafika kwa nia ya  kutoa mrejesho wa madai ya madaktari yaliyowasilishwa mezani kwake mnamo  tarehe 23.01.2012. Madai yetu yalikuwa manane na Mh Wazizri mkuu  aliweza kutoa maelezo ya dai moja baada ya lingine.

Miongoni mwa madai ambayo mpaka sasa yamepatiwa majibu ya kuridhisha ni pamoja na;

Kuwawajibisha  watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wakiwemo Katibu  Mkuu Mama Blandina Nyoni , na Mganga Mkuu wa Serikali Dr. Deo Mtasiwa. 

Aidha Mh waziri mkuu alisema kuwa ameshalifikisha kwa Mh Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania suala zima la kuwawajibisha watendaji wa wakuu  wa kisiasa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao ni; Waziri Mh  Hadji Mponda na Naibu Waziri; Mhe. Lucy Nkya.

Kama sehemu ya maridhiano, Mh Waziri Mkuu pia aliahidi mbele ya  mkutano kuwa hakutawepo na unyanyasaji au vitisho vya aina yoyote ile  kwa wale wote walioshiriki katika kushinikiza Serikali kutatua kero  hizo.

Aidha kama sehemu ya maridhiano, Mh waziri Mkuu pia alifuta zuio  la madaktari kutokufanya mikutano. Lakini pia, Mh waziri Mkuu alisema  kuwa Serikali haina kusudio la kumfukuza kazi mtumishi yeyote wa afya  yule kazi aliyeshiriki katika mchakato huu wa kuishikiniza Serikali  kutafuta ufumbuzi madai ya madaktari nchini.

Aidha, Mh waziri Mkuu amesema “Interns” wote waliokuwa wamehamishwa  kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamesharudishwa bila masharti  katika hospitali hiyo ili kuendelea na program kama kawaida. Hili pia  linaambatana na kulipwa na kupewa stahiki zao zote.

Pia suala la madaktari na familia zao kuwa na Kadi ya Bima ya Afya  ya kijani( Green Card) limekubaliwa na kwa sasa tusubiri utekelezaji.
Pia ilikubaliwa kuwa madaktari watapata fursa ya kukopeshwa magari kama watumishi wengine wa umma.
Mbali na madai hayo, pia Mh. Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya  madai yanayuhusu maslahi ya watumishi wa afya ikiwa ni pamoja na  Mishahara na Posho na stahiki mbalimbali.

Lakini hata, Mh waziri Mkuu  hakutoa majibu ya moja kwa moja ya kiwango gani kitakachoweza kulipwa na  Serikali kama mishahara, posho na stahiki mbalimbali kwa minajili  kwamba bado zinafanyiwa kazi na kamati ya wataalamu aliyoiunda ili  waweze kumshauri.

Aidha, Mh waziri Mkuu alisema kuwa kwa wakati huu  inaweza kupandisha “on call allowances” za kada mbalimbali za afya  kutoka shilingi 3,000 – 10,000/= na kufikia kati ya shilingi 5,000 hadi  25,000. Madaktari bado wanaona ongezeko hili halilingani na ukubwa wa  kazi ifanywayo pindi mtumishi wa afya anapokuwa “on call” na hivyo basi  kuendelea kupendekeza kuwa “on call” allowance iwe ni 10% ya mshahara  wa mtumishi husika.

Pia Mhe, Waziri Mkuu hakuweza kueleza kinagaubaga mkakati kazi wa uboreshaji wa huduma za afya wapatayo wananchi wa Tanzania. Baada  ya tamko hilo la Serikali kumalizika, Mh Waziri Mkuu na ujumbe wake  waliondoka, na Mkutano huo ukaendelea kwa Kamati kufanya Mkutano na  madaktari wote, lengo ikiwa kujadili tamko hilo na kutoa maazimio.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, madaktari walikubaliana kwamba;  kwa kuwa Serikali imeanza kuonyesha nia ya kutatua tatizo hili kwa  kutekeleza baadhi ya maazimio yetu, wajumbe kwa niaba ya madaktari wote  nchi nzima tulikubaliana na kuazimia yafuatayo;

- Kurudi kazini mara moja kuanzia kesho tarehe 10.02.2012 bila masharti yeyote.
- Kamati  ya jumuiya ya madaktari kama sehemu ya MAT kuendelea kukaa mezani ya  majadiliano na Serikali ili kuanza kupitia madai hasa yale yanayohusu  maslahi.

- Kukutana tena tarehe 03.03.2012 ili kupata mrejesho wa kiwango cha  utekelezaji wa madai hayo kwa mujibu wa vikao vya majadiliano na  makubaliano na hatimae kuchukua hatua zaidi.

- Kujadili utekelezaji juu ya Kuwawajibisha Waziri na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi na Jamii.

- Mwisho kabisa Madaktari wote kwa ujumla wake walilaani na kukemea  kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji wanaharakati wa haki  za kibinaadamu na mashirika ya kijamii wakiwemo Dr. Hellen Kijo-Bisimba  na Mama Ananilea Nkya na wanaharakati wengine wote waliokumbwa na kamata  kamata hiyo na hivyo basi tunalitaka jeshi hilo kuwaachilia huru mara  moja bila masharti yeyoye.
 
Pamoja Tunaweza
Imetolewa na Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari Tanzania
Dr. Ulimboka Stephen

No comments: