Tangazo

March 6, 2012

MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA: RUFAA ZA NTABAKUZE NA HATEGEKIMANA KUTOLEWA MEI 8

Aloys Ntabakuze
Na Shirika la Habari la Hirondelle,Arusha

 Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) itatoa hukumu za kesi mbili za rufaa zinazowahusu maafisa wawili wa zamani wa jeshi la Rwanda, Meja Aloys Ntabakuze na Luteni Ildephonse Hategekimana, Mei 8, 2012.

Kwa mujibu wa ratiba zilizotolewa Februari 29 na Machi 2, mwaka huu, Ntabakuza atakuwa wa kwanza kupokea hukumu yake akifuatiwa na Hategekimana. Maafisa hawa wanapinga adhabu za vifungo vya maisha walizopewa kutokana na kuhusika kwao katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini mwao.

Meja Ntabakuze ambaye alikuwa Kamanda wa Bataliani ya Makomando alitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita Desemba 18,2008, kutokana na askari waliokuwa chini ya mamlaka yake kushiriki kwenye mauaji yaliyofanyika maeneo ya Kabeza, Nyanza Hill na Chuo cha Takwimu (IAMSEA) mjini Kigali.

Kwa upande wake Luteni Hategekimana ambaye alikuwa Kamanda wa Kambi ndogo ya Kijeshi ya Ngoma mkoani Butare, Kusini mwa Rwanda alihukumiwa kifungo cha maisha jela Desemba 6, 2010 baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu kwa ushiriki wake katika mauaji ya watu kadhaa na kuamuru maauji ya kimbari dhidi ya Watutsi waliokuwa wanapata hifadhi katika kanisa la Ngoma.

Wakati wa kusikiliza rufaa ya Ntabakuze Septemba 27, 2011 na Hategekimana Desemba 6, 2011 upande wa utetezi kwa wote wawili waliomba wateja wao wachiwe huru kwa madai kwamba upande wa mashitaka umeshindwa kudhibitisha tuhuma pasipo kuacha mashaka.

Wakili Kiongzi wa Ntabakuze, Andre Tremblay, alieleza kwamba ‘’ushahidi uliotolewa na mwendesha mashitaka ni dhaifu mno kuweza kumtia hatiani na mrufani hakupata taarifa za kutosha kuhusiana na mashitaka aliyotiwa nayo hatiani.’’

Naye wakili Kiongozi wa Hategekimana, Jean de Dieu Momo alidai kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuunga mkono mashitaka dhidi ya mteja wake haukutoka kwa mashahidi walioshuhudia kwa macho yao uhalifu huo na badala yake ulikuwa ni ushahidi wa kusimuliwa tu na kwamba ulijaa uongo.

Kwa upande wake, mwendesha mashitaka aliiomba mahakama kuyatupilia mbali maelezo hayo ya mawakili wa utetezi kwa kile alichosema yamekosa uthabiti.

No comments: