Tangazo

June 19, 2012

MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA: Kapteni Nizeyimana ahukumiwa Kifungo cha Maisha

Kapteni Idelphonse Nizeyimana

 Na Hirondelle, Arusha

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne imemhukumu kifungo cha maisha jela afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kapteni Idelphonse Nizeyimana baada ya kumtia hatiani kwa kuhusika kwake kwa mauaji ya kimbari ya akiwemo Malkia wa mwisho wa Rwanda, Rosalie Gicanda.

Jaji Lee Muthoga aliyekuwa anaongoza jopo la majaji watatu, alitamka adhabu hiyo baada ya kumtia hatiani afisa huyo kwa kuamuru mauaji ya kimbari, kuteketeza kizazi na mauaji kama ukatili dhidi ya binadamu katika maeneo mbalimbali mkoani Butare, Kusini mwa Rwanda Aprili, 1994.

‘’Nizeyimana anahusika katika uhalifu wote huo kupitia ushiriki wake katika kundi la uhalifu,’’ alisema Jaji Muthoga.

Wengine waliouawa nje ya Malkia Rosalie ni pamoja na maelfu ya wakimbizi waliokuwa wanapata hifahdi ya maisha yao katika parokia ya Cyahinda na Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Rwanda, Pierre Claver Karenzi.

Majaji katika hukumu hiyo walikataa utetezi wa Kapteni Nizeyimana kwamba kati ya Aprili 20 na 22, mwaka 1994 na baadaye Aprili 26 hadi mwishoni mwa Mei, 1994 hakuwepo mkoani Butare.

‘’Utetezi huo hauaminiki na haupingani na ushiriki wa Nizeyimana katika mauaji ya kimbari,’’ majaji walieleza.

 Baada ya hukumu hiyo, John Philpot, Wakili Kiongozi wa Nizeyimana alisema atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo akidai kwamba ‘’ mahakama haikufuatilia kwa makini ushahidi ambao kwa kiasi kikubwa umetolewa na watu waliopangwa maalum kwa kazi hiyo kutoka nchini Rwanda.’’

Aliendelea kueleza kwamba ‘’mteja wetu alikuwa mpiganaji mzuri, askari mzuri aliyekuwa anaitetea nchi yake dhidi ya uvamizi na hakuwapo wakati mwingi yalipokuwa yanatokea matukio haya.’’

Mwendesha mashitaka pamoja na mambo mengine anadai kwamba mshitakiwa alikuwa mtu wa pili kimadaraka  aliyekuwa anashughulikia Usalama na Operesheni za Kijeshi katika Chuo cha Maafisa wa Jeshi Wasiokuwa na Kamisheni (ESO), mkoani Butare.

Nizeyimana alitiwa mbaroni nchini Uganda, Oktoba 5, 2009 na kuhamishiwa katika gereza la Mahakama ya Umoja wa Mataifa Arusha, Tanzania, siku iliyofuata.

Kesi yake ilianza kusikilizwa Januari 17, 2011 na kuhitimishwa Septemba 21, 2011.

No comments: