Tangazo

June 16, 2012

Nyumba ni ya Wema, si ya Wema?









ILIANZA chinichini kuwa fedha imemtembelea Wema Isaac Sepetu akithibitisha kumiliki nyumba ambayo ndani yake ina mazagazaga yanayoifanya kuwa na thamani ya Sh. milioni 400 lakini nyuma ya stori hiyo kuna zengwe, shuka na Ijumaa upate ‘udambwidambwi’ kamili.

Kwa mujibu wa chanzo kisicho na shaka ambacho ni mmoja wa mashosti wa Wema, nyumba hiyo anayotarajia kuhamia hivi karibuni ipo Mtaa wa Bwawani, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Kikifichua mambo mazito nyuma ya pazia, chanzo hicho kilidai kuwa watu wanaoijua ishu hiyo kiundani walipigwa na butwaa waliposikia Wema anamiliki mjengo huo wa kifahari huku wao wakielewa vingine.
 
“Ninavyojua ile nyumba siyo yake bali amepanga tu,” kilidai chanzo hicho na kuongeza:

“Aisee! Nimeshangaa kusikia Wema kanunua lile jumba wakati mchakato wa kwanza wakiwa na madalali walikuwa wakitafuta nyumba ya kupanga.

“Kusema kweli jambo lililonishangaza ni kuwa mpaka mchakato wa mwisho unafanyika kuhusiana na nyumba hiyo ni kwamba Wema alikuwa anaipangisha na siyo kuinunua.”

Wakati tukisikiasikia hayo, tukaletewa lingine jipya na sosi mwingine kuwa Wema alipewa jumba hilo lililokuwa likimilikiwa na mama Ngoma ili amalizie kurekodi filamu yake mpya ya The Superstar.

“Si mnakumbuka alivyofanya juzikati kwa kuvishwa pete ya uchumba na Mwinyi wa Machozi kumbe alikuwa anarekodi filamu, ndiyo hivyohivyo kwa hili jumba, kama hamuamini mtaona baadaye.

“Wewe angalia vizuri hizo picha, ni za filamu kabisa kwani kipande cha hiyo muvi kinamtaka aonekane akiishi maisha ya kistaa sana. Wewe nyumba gani umetenga mpaka chumba cha kuzungumza na vyombo vya habari?” alihoji sosi huyo.

Wakati mambo yakizidi kuwa mengi, kikaibuka chanzo kingine kikidai kuwa si kweli kwamba mjengo huo unamilikiwa na mama Ngoma bali ni ya Mwarabu fulani.

Baada ya kuambiwa vitu kibao kuhusu jumba hilo, Ijumaa lilianza kusaka ukweli ili kujibu maswali ya mashabiki wa Wema.

Mtu wa kwanza kuzungumza na Ijumaa ni meneja wa Wema, Martin Kadinda ambaye alikiri Wema kununua nyumba hiyo lakini si kwa Sh. milioni 400.

“Unajua huyo anayesema kuwa Wema amepanga siyo kwamba anakosea ila anachelewa kujua mambo.
“Ni kweli kabisa mara ya kwanza Wema alikuwa anataka kupanga nyumba hiyo lakini baadaye alikaa chini na mwenye nyumba na kukubaliana kufanya biashara ya kumuuzia lakini si kwa Sh. milioni 400,” alisema Martin.

Akifafanua fedha hizo zinazodaiwa kununulia mjengo huo, Martin alisema:

“Hiyo milioni 400 ni thamani ya nyumba na vitu vyote vya ndani. Siyo bei iliyonunuliwa.”

Ieleweke kuwa siyo kwamba hatumuamini Martin lakini tulizungumza na Wema ili mashabiki wake wamsikie mwenyewe.

Katika mahojiano maalum na Ijumaa, Wema alikiri kuwa anamiliki nyumba hiyo.

“Ni kweli namiliki nyumba hiyo ambayo ina thamani ya milioni 400, hao wanaosema nimepanga watajiju.
“Siwezi kununua fenicha za mamilioni ya shilingi halafu nishindwe kununua nyumba,” alisema Wema ambaye leo atakuwa jaji wa Shindano la Miss Dar City Center 2012 kwenye Hoteli ya Golden Tulip, Masaki jijini Dar.
Katika siku za usoni, Wema maarufu kwa jina la Pedeshee Mwanamke anapokuwa ukumbini kufuatia tabia ya kuwamwagia ‘mihela’ wanamuziki, amekuwa akifanya mambo makubwa yanayogharimu mshiko mrefu hivyo kuibua maswali mtaani.

Mfano, miezi kadhaa iliyopita alikwenda Dubai kufanya ‘shoping’ ya zaidi ya Sh. milioni 60, hajakaa vizuri akavuta mkoko mwingine tofauti ile Toyota Lexus Harrier unaoitwa Toyota Mark X huku akikamilisha filamu yake iliyogharimu Sh. milioni 68 kuitengeneza.

Weka hayo yote pembeni, anatarajia kufanya uzinduzi wa kampuni lake la filamu ambalo kila kitu kimekamilika.

Kufuatia kufuru hizo na nyingine ambazo hazijaorodheshwa hapo juu ndiyo maana kukaibuka maswali kuwa anapata wapi jeuri hiyo?

Madai ambayo huwa Wema hataki yaguswe ni kuwa eti ana mwanaume mwenye fedha zake aliyempata baada ya kuachana na mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond’.

Eti wanasema ndiye anayempa jeuri yote hiyo huku nyuma kukiwa na madai kuwa ni jamaa anayefanya kazi idara nyeti serikalini (tunalifanyia kazi tupeni muda kiduchu).Chanzo:Global Publishers

No comments: