Rais Dkt.Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe wakibeba jeneza la marehemu Bob Makani. |
Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wakitoa heshima za Mwisho. |
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpa pole Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Wilbroad Slaa katika viwanja vya Karimjee kufuatia msiba wa muasisi wa Chama hicho Bob Makani.
|
Rais Dkt. Jakaya Kikwete akiteta jambo na mjumbe wa tume ya kukusanya maoni juu ya katiba Prof.Mwesiga Baregu katika viwanja vya Karimjee leo. |
Rais Kikwete na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. (Picha zote na Freddy Maro) |
Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Juni 11, 2012, ameungana na mamia ya wakazi wa Dar es Salaam kuaga mwili wa aliyekuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Ndugu Bob Nyanga Makani.
Katika shughuli iliyofanyika kwenye Viwanja vya Ukumbi wa Karimjee mjini Dar Es Salaam, Rais Kikwete ameungana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Seif Sharrif Hamad na viongozi wengine wa Serikali na vyama vya siasa kuuaga mwili wa Ndugu Makani ambaye pia alipata kuwa Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha Chadema.
Miongoni mwa viongozi wakuu wa vyama vya siasa waliokuwepo kwenye shughuli hiyo ni Mheshimiwa Freeman Aikel Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha UDP, Mheshimiwa John Momose Cheyo.
Mheshimiwa Makani alifariki dunia mwishoni mwa wiki kwenye Hospitali ya Aga Khan mjini Dar Es Salaam kwa matatizo ya moyo na anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwao Shinyanga.
Katika salamu zake za rambirambi kwa familia kuomboleza msiba huo jana, Rais Kikwete alimwelezea Ndugu Makani kama Mtanzania mwadilifu na mzalendo ambaye alithibitisha sifa hizo katika nafasi zote alizopata kushikilia katika maisha yake iwe kwenye utumishi wa umma ama siasa.
……..Mwisho…..
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11 Juni, 2012
No comments:
Post a Comment