Tangazo

June 5, 2012

VIONGOZI WENGINE WAWILI WA UAMSHO ZANZIBAR WAJISALIMISHA POLISI

Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi, Zanzibar

ZANZIBAR JUMANNE JUNI 4, 2012.

VIONGOZI wengine wawili wa Jumuiya ya Uamsho Visiwani Zanzibar, leo wamefika Makao Makuu ya Upelelezi Zanzibar ambako walihojiwa kwa muda kuhusiana na vurugu za wiki iliyopita visiwani hapa kabla ya kuachiliwa.

Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amewataja Viongozi waliofika Polisi na kuhojiwa kuwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamshio Shekhe Mselem Bin Ali, mkazi wa Makadara na Shekhe Azan Ahmed Saidi, wa Mfenesini.

Inspekta Mhina amesema katika mahojiano hayo Polisi walibaini kuwa siku ya vurugu hizo, viongozi hao hawakuwepo mjini Zanzibar ingawa Polisi walitaka kujua zaidi kama wao walihusika katika maandalizi ya awali ya mpango huo kabla ya kuondoka kisiwani hapa.

Wakati wa matukio hayo Sheikhe Mselem alikuwa Pemba na Shekhe Azan alikuwa Uwarabuni kwa matibabu lakini alilazimika kurejea Zanzibar baada ya kusikia hali ya vurugu zilizofanywa na vijana wa kikundi chake.

Viongozi hao wanafanya idadi ya viongozi waandamizi wa Jumuiya hiyo waliojisalimisha na kuhojiwa kwa hiyari na Makachero wa Jeshi la Polisi mjini Zanzibar kufikia sita.

Jana viongozi wengine wanne kutoka katika kundi hilo la Uamsho, walijisalimisha wenyewe Polisi na kuhojiwa kwa masaa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa masharti.

Inspekta Mhina amesema kuwa bado Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa viongozi wengine wa Jumuiya hiyo ambao hawajafika Polisi, kufanya hivyo badala ya kusakwa na kutiwa nguvuni kuhusiana na vurugu hizo.

Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, walifika mjini Zanzibar na kuwataka wale wote waliohusika katika vurugu hizo kujitokeza kukabili mkono wa sheria.

Tayari watu 78 wamekamatwa na Polisi na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya vurugu zilizosababisha kuchomwa moto kwa magari na baadhi ya makanisa mjini Zanzibar.

No comments: