Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Idadi ya maiti za ajali ya kuzama kwa Meli ya MV Skagit zimeongezeka na kufikia 89 baada ya miili mingine 11 kupatikana leo katika maeneo manne tofauti ya visiwa vidogovidogo vilivypo mwambao wa Zanzibar.
Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa miili iliyopatikana leo, sita ni wanaume akiwemo kijana mdogo na mingine mitatu ya wanawake.
Inspekta Mhina amesema, maiti zote zimezikwa katika makaburi ya pamoja ya Kama yaliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar chini ya usimamizi wa Jeshi la la Wananchi wa Tanzanaia JWTZ, Jeshi la Polisi, MKMK, JKU na Varantia.
Amesema miili hiyo ilipatikana katika viisiwa vya Pungume, Fumba, Chumbe na eneo linalokupwa na kujaa maji la Funguyasini maeneo jirani na kisiwa mama cha Unguja.
Naye Mkuu wa Polisi Kikosi cha Wanamaji na Bandari Zanzibar SP Martin Lisu, amesema kuwa kunauwezekano mkubwa kuwa maiti hizo zinaibuka kutoka katika meli hiyo ya Skagit.
Kamanda Lisu, amesema kuwa kutokana na kuendelea kuibuka kwa maiti hizo, Maafisa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wanaendelea na zoezi lao la kutafuta miili mingine na kupokea taarifa za kuonekana kwa mwili kutoka kwa watu wenye vyombo binafsi vya uvuvi na kuzifuatilia.
Hivi karibuni akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, Daktari Mkuu Mwelekezi wa Jeshi la Polisi nchini Dk. Ahamed Makata, alisema kuwa maiti nyungi zitaweza kupatikana ifikapo siku ya nne tangu kuzama kwa meli hiyo.
Alisema tabia ya maiti ya binadamu aliyekufa maji na kuzama, haiwezi kukaa chini ya maji kwa muda mrefu kama haikufungwa na kitu kizito kabla ya kuzama.
"Kwa kawaida maiti ya mtu aliyekufa maji haiwezi kukaa ndani ya maji wakati wote na kwamba hata kama itaendelea kubaki majini lakini katika muda wa kuanzia siku tatu na nne mwili ama miili hiyo nilazima ianze kuibuka na kuelea juu ya maji". Alisema Dk. Makata.
MV Kalama |
MELI YA KALAMA YAPIGWA STOP
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeipiga marufuku meli ya MV Kalama ambayo ni pacha na meli ya Skagit iliyozama baharini wiki iliyopita.
Uwamuzi huo umetangazwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, wakati akipokea misaada ya fedha kutoka Mfuko wa Pensheni wa watumishi wa Serikali za Mitaa na Radio Coconut.
Balozi Iddi amesema kuwa pamoja na kuisimamisha meli hiyo kutoa huduma za usafiri kwenye bahari ya Hindi, pia imewataka watu wote wanaotaka kununua meli kuleta kwanza aina na muundo wa meli wanayotaka kuinunua na imetumika kwa muda gani.
Lakini amesema meli ambazo zimeshaingia na kusajiliwa, nazo zinafanyiwa uchunguzi ili kubaini ubora na umri wake tangu ianze kufanya kazi kabla ya kuingizwa nchini kwa biashara ya kusafirisha abiria.
Hata hivyo amesema kuwa Serikali inajipanga kununua meli ya uhakika itakayotoa huduma ya usafiri majini kati ya Zanzibar na Pemba na Zanzibar na dar es Salaam ili kupunguza mashaka kwa wasafiri.
Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali za Mitaa NLPF kupitia Mkurugenzi wake Bw. Andrew Kuyeyama umetoa shilingi milioni 5 na Bw. Ali Khatibu Dai wa Radio Coconut ametoa mchango wa shilingi milioni moja zote zikiwa kwa ajili ya kusaidia gharama za matibabu na za mazishi kwa wafiwa.
No comments:
Post a Comment