Tangazo

September 17, 2012

Twiga Cement yatoa somo kwa watengenezaji matofali.

Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Twiga Cement, Jayne Nyimbo (wa tatu kushoto), akikabidhi pipa la kuwekea maji kwa  Mkurugenzi wa Kampuni ya ufyatuaji Matofali ya VGK Ltd , Valence Msaki (kulia) aliyekuwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya utengenezaji matofali yaliyoandaliwa na kampuni hiyo kwa watengeneza matofali 210 jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kila mshiriki alipewa pipa moja. Kutoka kushoto ni, Meneja wa Matumizi ya Saruji Injinia, Danfrord Samwenda, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo,  Ekwabi Magigo na Meneja Udhibiti Ubora, Richard Magoda.

Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Twiga Cement, Jayne Nyimbo (kushoto), akikabidhi cheti kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya utengenezaji matofali, Maua Hamadi,  yaliyoandaliwa na kampuni hiyo kwa watengeneza matofali 210 jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto ni  Meneja Matumizi ya Saruji Injinia, Danfrord Samwenda na Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo,  Ekwabi Magigo.

Ofisa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Twiga Cement, Gloria Mabada akizungumza na mmoja wa washiriki wa mafunzo ya utengenezaji matofali, Valence Msaki katika mafunzo hayo ambayo washiriki 210 walihudhuria.

Baadhi ya washiriki 201 wa mafunzo ya utengenezaji bora wa matofali yaliyoandaliwa na Kampuni ya Twiga Cement jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
*************************************
Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Saruji ya Twiga ya jijini Dar es Salaam imeendesha mafunzo ya siku moja kwa wasambazaji wa saruji na wafyatua matofali 210 wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bi. Jayne Nyimbo alisema mbali na kutaka kuwa karibu na wadau hao wakubwa wa saruji, lengo la Kampuni ya Twiga ni kuhakikisha wadau hao muhimu wanafahamu jinsi ya kutengeneza matofali imara.

“Kampuni hii inachangia katika kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania huku pia ikichangia ujenzi wa taifa letu na ndio maana tunataka wafyatuaji wa matofali wafyatue matofali imara. Tumefanya hivyo kwa miaka yote 46 tuliyodumu kwenye soko la saruji nchini,” alisema Nyimbo.

Awali, akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja Udhibiti wa Ubora wa Kampuni ya Twiga, Richard Magoda alitoa historia ya saruji akisema ilianza kutumika huko Misri miaka mingi iliyopita kabla ya kuboreshwa Ulaya na kufikia kiwango cha sasa.

Aliwakumbusha wafyatuaji matofali kuwa saruji yenye ubora, mchanga safi usio na mizizi wala udongo na maji yasiyo na magadi au chumvi chumvi ni malighafi muhimu katika kupata tofali imara.

“Mfyatuaji anapaswa kuzingatia muda wa kuanza kuganda kwa saruji hivyo kutengeneza tofali kabla ya muda huo na kwa kuwa viwango vyetu vya saruji ni vya kimataifa na vimethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), tunaamini kuwa hayo yakizingatiwa tutakuwa na majengo imara yaliyojengwa kwa matofali yenye ubora,” alisema Magoda.

Aliwaambia washiriki hao kuwa Kampuni ya Saruji ya Twiga ina maabara yenye vifaa vya kisasa vya kuthibitisha na kuhakiki ubora unaotakiwa na kukidhi mahitaji ya wateja.

Meneja Matumizi ya Saruji, Danford Semwenda aliwasisitizia washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia viwango vya ubora vinavyokubaliwa na TBS kwa matofali yanayotumika Tanzania.

“Saruji ihifadhiwe sehemu kavu yenye mbao chini na isizidi miezi mitatu kabla ya kutumika. Kwenye maghala, mifuko ya saruji isiwekwe juu kwa zaidi ya mita moja, yaani mifuko 12 tu kwenda juu kwani saruji ikigandamizwa, hupungua ubora wake,” alisema.

Mafunzo hayo yaliyowashirikisha wakufunzi kutoka VETA, pia yalisisitiza katika utunzaji wa kumbukumbu za hesabu na uhakiki wa mali.

Baadaye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Nyimbo, alikabidhi vyeti kwa waliohudhuria mafunzo hayo na kutoa matanki  ya kuhifadhia maji kwa wafyatuaji matofali wote waliohudhuria mafunzo hayo ili yakawasaidie katika shughuli zao za kila siku na kuwaongezea ufanisi.

Hii ni mara ya nne mfululizo kwa Kampuni ya Saruji ya Twiga kutoa mafunzo kwa wajasiliamari na wasambazaji wa saruji huku wakilenga pia kwenda kufanya hivyo kwenye mikoa ya Dodoma, Mwanza na Arusha.

No comments: